ismailjussa

Archive for the ‘Kiswahili’ Category

Wagombea wa CUF waahidi neema Mji Mkongwe

In Kiswahili on September 30, 2010 at 12:07 am

Mgombea Uwakilishi wa Mji Mkongwe kwa tiketi ya CUF, Ismail Jussa, akiungana na wananchi kusherehekea uzinduzi wa kampeni za chama hicho katika jimbo hilo zilizofanyika Malindi (Kwa Sheha), Jumatatu ya tarehe 27 Septemba, 2010 (Picha kwa hisani ya Martin Kabemba)

Na Salma Said

VIJANA wa Mji Mkongwe Zanzibar wameahidiwa kupatiwa jumla ya shilingi millioni 81 za kununuliwa boti na mashine zake kwa matawi tisa ya mji huo na wagombea wa ubunge na uwakilishi muda mfupi baada ya kuapishwa endapo wataibuka washindi wa jimbo hilo.

Fedha hizo zimeelezwa kukabidhiwa kwa wananchi hao katika mkutano wa hadhara utakaofanyika siku chache baada ya kutangazwa washindi wa jimbo, Ibrahim Mohammed Sanya (Mbunge) na Ismail Jussa (Mwakilishi).

Akizungumza na wafuasi wa Chama Cha Wananchi (CUF) na wakaazi wa Mji Mkongwe, Sanya alisema fedha hizo ni ahadi kwake na ahadi kwa Mwenyezi Mungu ambapo alisema siku chache baada ya kuapishwa ataziwasilisha kwa vikundi hivyo ambavyo vitakuwa chini ya usimamizi wa kamati za maendeleo ambazo zitashirikisha vyama vyote vya siasa.

Akichambua matumizi ya fedha hizo alisema katika matawi hayo tisa kila tawi litanunuliwa boti na mashine za kuvulia samaki ili vijana waweze kujiajiri kwa kuuza samaki wengi.

“Ninaahidi kuwa mkisikia nimeshaapishwa tu kule Dodoma na Mheshimiwa Jussa ameapishwa Baraza la Wawakilishi basi tutaitisha mkutano mkubwa kuwakabidhi millioni 81 kwa matawi tisa na hili kama hatujalitekeleza basi…nawaruhusu mje kunitoa kwangu kwa mikwaju…” alisema na kuacha kicheko na vigeregere.

Akina mama kwa upande wao waliahidiwa kuendelezewa utaratibu wa kulipiwa fedha wanapotaka kujifungua sambamba na kutunziwa watoto wao kwa muda wa miezi sita tokea kuzaliwa kwa watoto hao kwa wakaazi wote wa Mji Mkongwe ambao hawana uwezo.

Mgombea huyo alisema sera ya CUF ni kuwasogezea wananchi wake huduma muhimu za maendeleo hivyo aliwataka wanawake kukiunga mkono chama hicho ili waweze kufunguliwa kituo cha huduma za akina mama waja wazito (Clinic) katika Mji Mkongwe ambao ni urithi wa kimataifa.

Sanya alisema wanawake wengi wanajazana Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja ambayo wananchi kutoka sehemu mbali mbali mjini na vijijini wanaitegemea hospitali hiyo lakini chini ya uongozi wa serikali ya umoja wa kitaifa itakayoongozwa na CUF itahakikisha inawasogezea huduma hiyo katika eneo lao la karibu badala ya kwenda Mnazi Mmoja.

“Hizi ahadi zetu ni za kweli, nasema kuanzia nitakapoapishwa tu iwe ni mwiko kwa akina mama kujifungua bila ya kupata zana za kujifungulia na mambo muhimu ya huduma yote tunataka tuwahakikishieni kuwa yatapatikana chini ya uongozi wetu…tupeni kura zenu ili tuwatumikieni” alisema Sanya ambaye anatetea nafasi yake ya ubunge katika jimbo hilo .

Akizungumza kwa hisia za kuwavuta vijana wengi, mgombea Uwakilishi wa Jimbo hilo, Jussa aliahidi kupambana na madawa ya kulevya na kuwaomba wazazi wa jimbo hilo kutowadharau vijana wao waliojiingiza kwenye utumiaji wa madawa kwani wengi wao hawakuingia kwa hiari bali ni kunatokana na kukosa ajira na kukata tamaa za maisha.

Alisema vijana wengi wamemaliza masomo yao lakini kutokana na umasikini wa wazazi wao wameshindwa kuwaendeleza jambo ambalo limechangia vijana hao kujiingiza katika matumizi ya madawa ya kulevya.

“Vijana wamekuwa adha kwa familia, adha kwa jamii na adha kwa yeye mwenyewe, na baadhi yao wameingia sio kwa kupenda lakini kutokana na maisha kuwa magumu na kukata tamaa. Lakini tunakuahidini vijana tutawapa kila support waondokane na madawa haya” aliahidi Jussa na kuongeza kwamba iwapo hadi hizo hazikutekelezwa kwa muda mfupi basi wananchi wasiwachague tena katika chaguzi nyengine zitakazofuata.

Aidha alisema sekta nyengine muhimu ya kuangaliwa ni elimu ambapo asilimia kubwa ya vijana wa Mji Mkongwe hushindwa kuendelea na masomo ambapo aliahidi kuzindua Mfuko wa Amana kwa ajili ya Maendeleo ya Elimu katika Jimbo la Mji Mongwe (Stone Town Education Trust Fund) wa kuwaendeleza vijana wasiokuwa na uwezo.

Alisema kazi za Mfuko huo zitakuwa ni kuhakikisha hakuna kijana atakayekosa elimu kutokana na umasikini wa wazazi wake na vijana ambao wameshindwa kujiendeleza kielimu watapatiwa mafunzo ya kazi za ufundi ambapo aliahidi kufungua kituo maalum cha mafunzo ya kazi za amali.

“Tutafungua kituo maalum cha kazi za amali na tutawapa mafunzo na wakihitimu tu mafunzo yao kila mwanafunzi atakabidhiwa kisanduku cha zana zake (tool kit) za kufanyia kazi na watu wanaotaka kufanyiwa kazi watakuja pale kuwafuata.

Akiwageukia akina mama, Jussa alisema watawezeshwa ili waweze kufanya biashara ndogo ndogo zitakazowasaidia kuondokana na utegemezi kwa waume zao.

“Akina mama muweze kuuza biashara zitakazowanufaisha na msiishie kuuza ubuyu na chips za mihogo tu ingwa tunajua bidhaa hizo zinauzwa na zinatafutwa hadi Ulaya lakini mjishughulise na bishara nyengine za ufundi zikiwemo biashara za kutengeneza bidhaa za kazi za mikono” alisisitiza Jussa huku akipigiwa vigeregere.

Mgombea Uwakilishi huyo alisema Mji Mkongwe licha ya kuwa ni urithi wa kimataifa lakini umekosa haiba yake kutokana na bidhaa zinazouzwa katika mji huo kuwa haziendeni na asili yake kutokana na kuzagaa kwa vinyago katika maeneo yote ya mji huo.

Alisema asili ya mji mkongwe ni bidhaa za asili zinazotengenezwa kwa mikono lakini hivi sasa kumejaa vinyago jambo ambalo linapoteza sura na haiba ya Mji Mkongwe ambao ni maarufu duniani kote.

 

Source: Mzalendo.net

Advertisements

CUF: Tutatenga asilimia 25 ya bajeti katika elimu 2010-2015

In Kiswahili on September 7, 2010 at 10:09 pm

Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CUF, Prof. Ibrahim Lipumba, akifafanua sera za chama chake katika moja ya mikutano ya chama hicho.

Tuesday, 07 September 2010 08:59

 Na Zaina Malongo

CHAMA cha Wananchi (CUF) kupitia ilani yake ya uchaguzi inayoitwa ‘Rais Makini, Serikali makini,Uchumi imara na Mabadiliko sahihi’ kinasema kukua kwa uchumi wa kisasa na wenye uwezo wa kuboresha maisha ya wananchi kunategemea kuwepo kwa wafanyakazi wenye ujuzi na maarifa.Ilani inaongeza kusema kuwa Watanzania  hawataweza kushindana kiuchumi na kibiashara katika ulimwengu wa sasa kama hatua za makusudi hazitochukuliwa  kuhakikisha kuwa wananchi   wengi  wanapata fursa za elimu.

Ni kwa sababu hii chama hicho kinaahidi kutenga asilimia 25 ya bajeti ya kila mwaka katika kuendeleza sekta ya elimu.Ufuatao ni muhtasari wa ahadi muhimu zilizomo katika ilani hiyo iliyozinduliwa hivi karibuni.

Elimu ya msingi na chekechea

CUF inaahidi kuhamasisha ujenzi wa shule binafsi na kufuta kodi katika vifaa vya elimu, kufanyia marekebisho ya mitalaa, kuhimiza matumizi ya kompyuta shuleni, kutoa lishe kwa wanafunzi, kutoa elimu bure na kupiga marufuku michango ya aina zote, kuboresha huduma  za ukaguzi na kuongeza mishahara na ujenzi wa  makazi bora ya walimu.

Elimu ya sekondari

Ilani inasema ongezeko la bajeti ya elimu kwa jumla litakipa chama uwezo wa kufanya marekebisho yanayohitajika. Serikali  itachukua hatua zifuatazo ili kuyafikia malengo yake kwa kutoa elimu ya sekondari bure. Malengo haya ni pamoja na  kuhamasisha ujenzi wa shule binafsi, marekebisho ya mitaala, kuboresha  huduma za ukaguzi na kuongeza maslahi ya walimu na makazi bora.

Elimu ya juu

Pamoja na kwamba Serikali ya CUF imedhamiria kutumia si chini ya asilimia 25 ya bajeti kuboresha elimu nchini, Serikali pia itachukua hatua zifuatazo kuhakikisha kuwa malengo haya yanatimizwa;
Kugharamia mahitaji ya wanafunzi wa elimu ya juu, kutoa posho za kujikimu vyuoni na wakati wa mafunzo kwa vitendo zinazokidhi mahitaji,kukuza matumizi ya intaneti katika vyuo vikuu, kila chuo kikuu cha umma kuwa na makazi thabiti ya wanafunzi.

Hatua nyingine ni wahadhiri kupewa nyumba na mshahara unaokidhi hali halisi, uboreshaji wa mitaala, kuongeza nafasi zaidi za masomo ya Sayansi na Teknolojia, kuimarisha huduma za kitafiti, ujenzi wa miundombinu katika vyuo vikuu vyote, maktaba zenye uwezo mkubwa.

Elimu maalum kwa walemavu

Kwa kutambua umuhimu mkubwa wa kuwaendeleza watoto wenye ulemavu na kuwapunguzia wazazi mzigo wa ziada katika kuwahudumia, serikali ya CUF itachukua hatua zifuatazo:

 Itazindua sera mpya ya elimu ambayo itakuwa imeyajumuisha kwa ukamilifu mahitaji maalum ya wanafunzi wenye ulemavu na kufanya marekebisho mbalimbali ya kiufundi kwenye taasisi mbalimbali za elimu ili kuondoa vikwazo mbalimbali vinavyowakwaza wanafunzi wenye ulemavu wanaosoma katika taasisi hizo.

Nyingine ni kujumuishwa kwa mahitaji maalum ya kielimu kwa watoto wenye ulemavu  katika mitaala ya vyuo vya ualimu ili kuongeza idadi ya walimu wenye uwezo wa kutoa elimu kwa watoto wenye ulemavu na kugharamia kwa asilimia mia moja gharama zote zinazohusiana na masomo ya wanafunzi wenye ulemavu katika ngazi zote za elimu.

Elimu ya watu wazima

 Serikali ya CUF itahuisha upya madarasa ya elimu ya watu wazima. Serikali itaandaa utaratibu utakaowezesha kila shule ya msingi iliyoko nchini kuendesha madarasa ya elimu ya watu wazima kila siku jioni kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa. Kwa hali hii fedha za bajeti ya elimu ya watu wazima zitatumika ipasavyo na hivyo kuwanufaisha walengwa.

Serikali ya CUF itafuta ada zote zinazotozwa na maktaba za serikali hivi sasa na kuhakikisha kuwa huduma katika maktaba hizi zinaboreshwa kwa kiwango cha juu ili kukidhi haja ya wananchi kujiendeleza kielimu. Maktaba zitaunganishwa na mtandao wa intaneti.

Elimu ya Ufundi

Serikali ya CUF inataka kuona elimu ya ufundi inakuaa nyenzo muhimu ya maisha kwa vijanaa. Kutekeleza hili inakusudia kuongeza shule za ufundi  kila wilaya kwa kadri ambavyo uchumi wa nchi unavyokua na serikali itazisimamia ipasavyo.

Inaahidi kuwa kila  mtoto asiyejiunga shule ya sekondari lazima apate nafasi ya kusoma masomo ya ufundi ili ajijengee mazingira ya kupata ajira au kuwa na uwezo wa kujiajiri katika sekta binafsi.

Jambo jingine serikali itawapeleka walimu wengi zaidi katika mafunzo ya juu ya ufundi ili vyuo vya ufundi viwe na wataalam wa kutosha watakaokuwa wakiwafundisha wanafunzi kwa kuzingatia msisitizo wa mafunzo kwa vitendo kuliko nadharia.

Source: Mwananchi

Jino kwa jino CUF, CCM na Chadema

In Kiswahili on September 6, 2010 at 10:36 pm

Ukurasa wa mbele wa gazeti la 'Raia Mwema' ukiripoti mwenendo wa kampeni za vyama vikuu vya siasa hapa nchini.

 
Na Mwandishi Wetu
 

WAKATI vumbi la kampeni likiendelea kutimka, Chama  Cha Wananchi (CUF) kimelalamikia mwenendo wa kampeni wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama Cha Mapinduzi (CCM), malalamiko yanayohusisha kauli za vyama hivyo na matumizi ya fedha.

Mbali na malalamiko hayo, Mgombea Mwenza wa CUF, Juma Duni Haji, amedai kukutana na vituko alivyoviita vya Serikali ya Rais Jakaya Kikwete.

Kwa mujibu wa Duni Haji, vituko hivyo ni pamoja na kukuta shule yenye Mwalimu mmoja ambaye ndiye Mwalimu Mkuu na alipomuuliza kwa nini anajiita Mwalimu Mkuu, aliambulia kicheko kutoka kwa mwalimu huyo.

Akizungumza na Raia Mwema kwa simu kutoka mkoani Kagera, Msemaji wa Kampeni za CUF, Mbarara Maharagande, alishangazwa na ujasiri wa CCM kutumia mabilioni ya fedha kiasi cha kupindukia kwenye kampeni zake, wakati huduma za jamii zikizidi kuwa duni kwenye maeneo wanakojinadi.

“Athari kubwa ambayo inatukabili ni matumizi makubwa ya fedha kwa upande wa CCM, tupo njiani kuelekea Bukoba Vijijini ni dhahiri fedha nyingi zimetumika na hii ni njia mojawapo ya kukandamiza demokrasia,”

Alipoulizwa kwamba matumizi ya fedha hizo inawezekana ikawa kwa mujibu wa Sheria ya Gharama za Uchaguzi inayotaja kiwango hadi Sh bilioni 50, Maharagande alisema kwa vyovyote vile na hasa kwa kuzingatia mazingira ya Tanzania, demokrasia inaathirika.

“Wamesambaza mabango kila kona, fulana zitagawiwa karibu kwa kila Mtanzania…najiuliza inakuwaje mabilioni yamwagwe kiasi hicho wakati huduma za jamii kule wanakoenda kuomba kura zikiwa zimezorota. Dawa hospitalini hakuna hata karatasi za kuandika taarifa za wagonjwa lakini karatasi za kampeni zimesambazwa hadi vyooni,” alisema Maharagande na kuongeza kuwa wana matarajio makubwa kwamba Profesa Ibrahim Lipumba mgombea urais kwa tiketi ya CUF atashinda na kuunda serikali licha ya matumizi hayo makubwa ya fedha kwa upande wa CCM.

Katika hatua nyingine, Maharagande alikilalamikia CHADEMA akisema kimekuwa kikitumia lugha za kashfa dhidi ya wagombea wengine bila kujali ni wa CUF au chama kingine.

Alibainisha kuwa kitendo cha mgombea urais wa CHADEMA, Dk. Wilibrod Slaa kuzungumzia posho, mishahara na mafao ya wabunge kuwa ni makubwa na kutumia ajenda hiyo kwenye kampeni ni usaliti.

Alisema Dk. Slaa ni sehemu ya viongozi waliopitisha mafao hayo kwa kuwa alikuwa Naibu Kiongozi wa Upinzani pamoja na Mbunge wa CUF, Hamad Rashid Mohamed na kwamba Dk. Slaa mwenyewe alichukua mafao na mishahara hiyo ya wabunge anayodai ni mikubwa.

Mbali na kulalamikia hoja hiyo ambayo inaelekea kukikera CUF, Maharagande alisema CHADEMA pia imejihusisha na vitendo vya vurugu dhidi ya chama chake.

“CHADEMA walimshambulia mgombea wetu wa ubunge Tarime (Charles Mwera) na hivi karibuni wametoa lugha za kashfa kwa wagombea wa chama kingine….huu si ustaarabu, tunawashauri waache mwenendo huo,”

Alipoulizwa ni kwa nini ameanza kuwa na mwelekeo wa kutetea wagombea wa CCM ambao hivi karibuni ndio waliodaiwa kushambuliwa na viongozi wa CHADEMA, alisema CUF ina haki ya kutoa msimamo wake kuhusu masuala ya msingi yanayoweza kuathiri mwenendo wa nchi.
  
Malalamiko dhidi ya CHADEMA yamekwishatolewa na CCM, kupitia mwenyekiti wa kampeni za chama hicho, Abdulraham Kinana, akidai kusikitishwa na maelezo ya wakili mwandamizi nchini, Mabere Marando aliyesema Mgombea wa CCM, Jakaya Kikwete, Rostam Azizi na Edward Lowassa wanahusika kwenye wizi wa mabilioni ya fedha kutoka Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) Benki Kuu ya Tanzania.

Katika mazungumzo yake na Raia Mwema Jumanne wiki hii, Kinana alishauri CHADEMA watumie hoja kushawishi wapiga kura na si kuzusha kashfa, kuhangaika kuweka pingamizi au kukimbilia mikutano na waandishi wa habari, akisisitiza ni muhimu kukimbilia kujinadi kwa wapiga kura ili kueleweka na kuchaguliwa.
 
“Siku hizi za awali kwa mujibu wa kampeni zetu kuna kila dalili za ushindi mkubwa kwa sababu tunaeleza tulichofanikiwa kufanya na tutakachofanya tukiendelea kuchaguliwa, wananchi wanatuelewa vizuri,”

“Hali hiyo ni tofauti na wenzetu ambao wanaendeleza yale ya miaka 15 iliyopita ya kufanya kampeni za kuzua kashfa, waeleze watafanya nini,” alisema Kinana.

Katika hatua nyingine, Mgombea Mwenza wa CUF Juma Duni Haji alilieleza gazeti hili kwamba Watanzania waelewe kuwa hata wakiipa CCM miaka mingine 100 ya kutawala hawataweza kuwa na maisha bora.

“Kuna silaha mbili zinazotumiwa na CCM kushinda. Kwanza, masikini na mtu mjinga ndiye anayetawalika. Pili, tajiri hawezi kutawalika. Kwa hiyo wanatambua hizi silaa na wanahakikisha watu wanabaki kuwa masikini na wajinga ili waendelee kutawala.

“Tumefika kwenye shule moja tumekuta ina wanafunzi 900 lakini walimu wanne, kwenye shule nyingine mwalimu mmoja huyo huyo amejiita Mwalimu Mkuu, ukimuuliza kwa nini ajipe cheo hicho anacheka  tu,” alisema Duni.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni za CHADEMA, Profesa Mwesiga Baregu, amemjibu Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba na Kinana, akisema kwamba hakuna kiongozi wala mgombea wa chama chao aliyetoa matusi ama kufanya vurugu bali kinachotokea ni CCM kutapatapa.

Akizungumza na Raia Mwema kwa njia ya simu jana, Profesa Baregu amesema anashangazwa na kauli kwamba CHADEMA imetoa matusi na kufanya vurugu katika kampeni zake za hivi karibuni.

“Tangu tulipokuwa kwenye mkutano wa kuzindua kampeni, hakuna mzungumzaji aliyetoa matusi ama kufanya vurugu.  Wanashindwa (CCM) kutenganisha kati ya matusi na kusema ukweli, maana kilichozungumzwa ni kwamba kesi za EPA zilizopo mahakamani hazitoshi na waliohusika moja kwa moja hawajaonekana na wakatajwa. Hakuna matusi hapo,” alisema Baregu.

Baregu alizungumzia pia kuhusu kauli ya Makamba kudai kwamba Mgombea Urais wa CHADEMA, Dk. Wilbroad Slaa haaminiki akisema kwamba hayo maneno hayo ni dalili ya kutapatapa.

“Kuna mazungumzo mengine kama ya Makamba anaposema Dk.Slaa haaminiki na kwamba kaasi dini na kaasi mke wake. Hayo sijui ana uhakika gani? Slaa hana ugomvi na Kanisa Katoliki  na ndiyo maana alihusika kupanga safari ya Papa (John Paul II) alipokuja Tanzania.

“Hapa ukweli ni kwamba alishindwa taratibu za upadri na ni uaminifu si ukosefu wa uaminifu ndiyo maana aliomba ruhusa ya Kanisa Roma na akakubaliwa, kusema ukweli ndiyo uaminifu na ndiyo maana alikubalika. Anataka awe mnafiki aende kanisani mchana halafu usiku aende mtaani kubangaiza,” alisema Baregu.

Source: Raia Mwema

Maalim Seif asema yuko tayari kuiongoza Zanzibar mpya

In Kiswahili on September 2, 2010 at 2:16 pm

Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Wananchi (CUF) ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, akisalimiana na Bw. Alan Winde, Waziri wa Fedha, Maendeleo ya Uchumi na Utalii wa Serikali ya Western Cape ofisini kwake wakati wa ziara maalum ya mafunzo ya kikazi iliyofanyika wiki iliopita. (Picha kwa hisani ya FNF)

 

Imetolewa na CUF Makao Makuu

Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Wananchi (CUF) ambaye pia ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, juzi amerejea kisiwani Zanzibar akitokea Afrika Kusini ambako alikuwa na ziara maalum ya mafunzo ya kikazi yaliyolenga kumuandaa na majukumu mapya ya kuongoza Serikali baada ya uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 31, mwaka huu.

Ziara hiyo maalum ya siku nne ilikuwa kati ya tarehe 26 hadi 29 Agosti na iliandaliwa kwa mashirikiano baina ya Chama cha CUF, Taasisi ya Friedrich Naumann Stiftung ya Ujerumani na Chama cha Democratic Alliance (DA) cha Afrika Kusini. Maalim Seif alikuwa mgeni wa Serikali ya Jimbo la Western Cape ambayo inaongozwa na chama cha DA.

Akiwa katika ziara hiyo maalum ya mafunzo ya kikazi, Maalim Seif alikutana na kufanya mazungumzo na kubadilishana mawazo na viongozi na maafisa mbali mbali waandamizi wa Serikali ya Western Cape pamoja na Jiji la Cape Town.

Miongoni mwa viongozi na maafisa waandamizi aliokutana nao ni pamoja na Bw. Alan Winde, Waziri wa Fedha, Maendeleo ya Uchumi na Utalii wa Serikali ya Western Cape.

Maalim Seif pia alikutana na Ryan Coetzee, Mshauri Maalum wa Waziri Mkuu wa Jimbo la Western Cape, Christy Kirkpatrick, Mkurugenzi Mtendaji wa Kitengo cha DA cha Kusaidia Serikali yake kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, James Selfe MP, Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Taifa la DA, na Nick Clelland-Stokes, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano katika Ofisi ya Waziri Mkuu wa Western Cape.

Wengine ambao Maalim Seif alikutana nao ni Madiwani wanne wa Jiji la Cape Town wanaotoka chama cha DA ambao pia wanasimamia Wizara Maalum, Grant Pascoe (anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii) Felicity Purchase, (anayeshughulikia Maendeleo ya Uchumi na Utalii), Belinda Walker, (anayeshughulikia Huduma kwa Makampuni makubwa ya Biashara na Uendelezaji wa Rasilimali Watu), na Ian Neilson, Naibu Meya Mtendaji na pia anashughulikia Fedha.

Ziara ya Maalim Seif ilimalizika kwa kukutana na Paul Boughey, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu ya Western Cape na David Maynier MP, Waziri Kivuli wa Ulinzi na Wastaafu wa Jeshi katika Bunge la Taifa la Afrika Kusini.

Mambo yaliyohusika katika ziara hiyo maalum ni pamoja na vipi Serikali za kisasa zinaendeshwa, umuhimu na mambo yanayohitaji kufanya maamuzi magumu katika kipindi cha mpito, uwajibikaji na ufanisi katika serikali za kisasa, mipango ya maendeleo ya kiuchumi na maamuzi ya vipaumbele katika utayarishaji wa bajeti, serikali za pamoja (zinazojumuisha chama zaidi ya kimoja) zinavyofanya kazi, changamoto zake na mafanikio yake, ugawaji wa wizara na majukumu na utendaji kazi katika serikali za pamoja, na jinsi ya kutatua migogoro pale inapozuka kwenye serikali ya pamoja.

Katika ziara hiyo, Maalim Seif alifuatana na Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa kuteuliwa na Rais aliyemaliza muda wake na pia mgombea uwakilishi katika jimbo la Mtoni kwa tiketi ya CUF.

Akizungumzia ziara hiyo mara baada ya kuwasili kutoka Western Cape, nchini Afrika Kusini, Maalim Seif alisema:

“Nimefarijika na nimefaidika sana na ziara hii ya mafunzo ya kikazi na nawashukuru sana chama cha DA ambacho ni chama mshirika wa CUF katika Mtandao wa Vyama vya Kiliberali Duniani na ule wa Afrika.

Nimevutiwa mno na jinsi Serikali ya Western Cape inavyofanya kazi zake kwa ufanisi na uwajibikaji wa hali ya juu chini ya uongozi wa Waziri Mkuu wake, Mheshimiwa Helen Zille kiasi cha kulifikisha jimbo hilo kuwa ndilo linaloendeshwa vizuri kuliko yote nchini humo. Wamefanikiwa sana kubadilisha hali za maisha ya watu wake.

Nimejifunza mengi kuhusiana na mfumo wa serikali za pamoja zinazojumuisha chama zaidi ya kimoja zinavyofanya kazi hasa ukizingatia kuwa kuna maeneo katika Serikali ya Shirikisho ambayo chama ca DA kinapaswa kushirikiana na ANC.

Nimerudi na ari kubwa sana ya kuona nayatumia mafunzo hayo wakati ninapojiandaa kuiongoza Zanzibar Mpya pale Wazanzibari watakaponipa ridhaa kupitia uchaguzi mkuu, lengo likiwa ni kutekeleza sera zetu zilizomo katika Dira ya Mabadiliko ya CUF tutakayoizindua wakati wa kampeni.”

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa wa CUF, Ismail Jussa, alisema:

“Kwa niaba ya CUF na Ofisi yangu nawashukuru kwa dhati Taasisi ya Friedrich Naumann Stiftung kwa kupokea ombi letu na kuandaa programu safi kama hii.

Maalim Seif ambaye tunaamini ana nafasi kubwa sana ya kuapishwa kuwa Rais wa Zanzibar mara baada ya Oktoba 31 amerudi na furaha kubwa sana kutokana na tija waliyoipata yeye na Mhe. Mazrui na tayari ameagiza kufanyika kikao maalum cha kutoa maelekezo kuhusu mambo ambayo timu ya CUF inapaswa kujiandaa nayo katika kuitumikia Zanzibar Mpya.

Ni makusudio yetu kuendelea kutafuta fursa za ziara maalum za mafunzo ya kikazi kama hizi ili kuendelea kuwajengea uwezo viongozi wetu na kuwatayarisha na changamoto kubwa zinazotukabili kutokana na matarajio makubwa yanayoonekana kujengwa na Wazanzibari kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa itakayoundwa mara baada ya uchaguzi mkuu.”

 

Zanzibar

1 Septemba, 2010

 

CUF ‘kushambulia’ kutokea ardhini

In Kiswahili on August 25, 2010 at 10:30 pm

Mgombea Ubunge katika jimbo la Morogoro Mjini kupitia chama cha CUF Abeid Mlapakolo, akIzungumza katika mkutano wa kampeni wa chama chake katika kitongoji cha Masuka jana,huku akiwa ameshikilia picha za mgombea Urais kwa tiketi ya Chama hicho Prof. Ibrahim Lipumba na mgombea mwenza Juma Duni. (Picha kwa hisani ya Juma Mtanda wa The Citizen/Mwananchi)

24 August 2010

Na Ramadhan Semtawa

WAKATI vyama vya CCM na Chadema vikiwa vimetangaza kampeni za angani, CUF imetangaza kuwa itashambulia kwa kutokea ardhini, huku ikimtaka Zitto Kabwe akae chonjo kwenye Jimbo la Kigoma Kaskazini.

CUF imetangaza mkakati huo jana, ikieleza kuapnai kuzibomoa ngome za CCM na Chadema kwenye Jimbo la Kigoma Kaskazini kwa kuwachukua makada wake maarufu, akiwemo Sijapata Nkayamba, aliyekuwa mbunge viti maalumu wa chama hicho tawala.

Akitangaza mpango mzima wa kampeni za chama hicho zitazozinduliwa Ijumaa kwenye Uwanja wa Kidongo Chekundu, mkurugenzi wa siasa wa CUF, Mbaralah Maharagande alisema uamuzi huo umezingatia kwa kina tathmini ya kampeni katika vipindi vyote vya nyuma.

“Tumefanya tathmini katika chaguzi zilizopita kuanzia mwaka 1995, 2000 na 2005, tulibaini kulikuwa na makosa, kwa hiyo hatutaki tena kurudia makosa yale yale katika kampeni,” alisema Maharagande.

“Kwa hiyo… tutatumia nchi kavu; kuweka kambi na kuelimisha vema watu wetu wasimamie kura kuhakikisha haziibwi na mawakala wa usimamizi wa uchaguzi. Tuna mtandao hadi vijijini… hiki si chama cha promotion sawa na bidhaa mpya.

“Tutafanya kampeni za kistaarabu… tumeona unaweza kutembea juu, lakini huku chini kura zikakosa wasimamizi wa kutosha. Sisi tumejifunza na hatutaki kufanya makosa tena.”

Alifafanua kwamba baada ya uzinduzi wa kampeni zao, msafara wa viongozi wa CUF utakuwa tayari kusambaa maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kufanya kile alichokiita mashambulizi ya nchi kavu ya kuing’oa CCM Oktoba 31.

Maharagande alisema Agosti 27, msafara tofauti ya viongozi wa chama hicho, ikiongozwa na mgombea wao wa urais, Profesa Ibrahim Lipumba na mgombea mwenza Juma Duni Haji, itaanza kuelekea mikoani.

Katika ratiba hiyo, Maharagande alisema Profesa Lipumba ataanzia mkoa wa Pwani kwa kupita Kibiti, Ikwiriri na baadaye kuelekea Kilwa, Lindi na ukanda mzima wa kusini huku mgombea mwenza akianzia Kagera. Alijigamba kwamba wanayo magari ya kutosha ya msafara na yale ya uhamasishaji.

Alitamba kwamba sababu za kutumia kampeni za nchi kavu wanazo ikiwa ni pamoja na mtandao wake mkubwa katika ngazi za vijiji na mitaa na kuongeza kuwa “CUF si chama cha promotion kama vile bidhaa mpya”.

“Ni chama ambacho kimejikita vema hadi vijijini… hata katika uchaguzi wa serikali za mitaa baada ya CCM ni CUF. Ni chama ambacho mgombea urais alifahamika mapema, siyo chama ambacho bado siku 72 kwa uchaguzi mgombea urais hajulikani, na kubaki kudhani mara mgombea mwenza atakuwa Hamad Rashid; sijui nani; hatuko hivyo.”
         
“Tutafanya kampeni kitongoji kwa kitongoji; tutaweka kambi kuhakikisha watu wanasimamia vema; watu wetu lazima waelewe kulinda kura kwanza; siyo unapaa angani wakati chini kura zako hazina msimamzi wala huna mtandao. CUF chama kubwa.”

Akizungumzia programu nyingine, alisema keshokutwa pia chama hicho kitazindua Ilani yake katika hafla ambayo watu mbalimbali wamealikwa na kwamba ilani hiyo  inatoa dira ya mabadiliko nchini.

Maharagande alisema ilani hiyo itaonyesha ni kwanini ilikuwa ni makosa kuendelea kuipa CCM nafasi ya kuongoza na kusababisha umasikini katika miaka yote 49 ya uhuru.

Katika hatua nyingine, CUF imefanikiwa kuzibomoa ngome Chadema na CCM mkoani Kigoma kwa kuchukua makada maarufu ambao wanakiweka chama hicho katika nafasi nzuri ya kuweza kutwaa majimbo mawili mkoani humo.

Nkayamba, ambaye aliangushwa kwenye kura za maoni ndani ya CCM kwa kuwa mtu wa nne na kuhamia CUF, anawania ubunge wa viti maalumu Kigoma Kaskazini, huku mshindi wa pili wa kura za maoni kutoka chama hicho tawala naye akijiunga na chama hicho cha upinzani na kuwa mgombea wa jimbo hilo ambalo linawaniwa pia na Zitto.

Akitangaza ujio wa wanachama hao, naibu mkurugenzi wa habari wa CUF, Ashura Mustafa alisema Zitto akae chonjo kwa kuwa ngome hiyo sasa imehamia CUF kutokana pia na kada maarufu wa Chadema na diwani kwa miaka 15 katika kata  yenye watu wengi ya Mwandiga, kuhamia chama hicho pinzania.

Omar Musa Nkwarulo, ambaye alikuwa mshindi wa pili katika kura za maoni CCM, alisema ameamua kukihama chama hicho tawala kutokana na siasa za kubebana na kuonya hizo ndizo zitachangia kifo cha CCM.

Nkwarulo alidai kuwa ana uhakika alikuwa ameshinda kwenye kura za maoni CCM, lakini kura katika eneo alikozaliwa lenye watu karibu 2,500 hazikuhesabiwa kwa kile alichokiita kuwa ni chama kumbeba mgombea mwenzake.

Alitamba kwamba kutokana na nguvu na ushawishi mkubwa wa kisiasa alionao ana uhakika wa kulinyakua jimbo hilo huku akimpa onyo Zitto kwamba ataanguka kutokana na kusahau jimbo hilo na kuliacha likiwa na umasikini wa kutisha.

CUF pia imemnyakua Optatus Likwelilo kutoka CCM ambaye naye atasimama kugombea ubunge Jimbo la Kigoma Kusini, huku akitamba kulinyakua kutoka katika chama hicho tawala.

Kwa upande wa Nkayamba alisema CCM ni chama ambacho kimejaa mizengwe huku akisisitiza kwamba licha ya kuwa mshindi wa tatu bado alitupwa hadi nafasi ya nne katika mchakato wa kuwania jimbo hilo.

Naye diwani huyo wa muda mrefu wa Chadema wa tarafa hiyo ya Mwandiga alikituhumu chama hicho kuwa kimejaa makundi, ubinafsi ambao unaanzia kwa uongozi wa ngazi ya juu.

 

SOURCE: Mwananchi

Viongozi wa CCM Kigoma wajiunga na CUF

In Kiswahili on August 19, 2010 at 10:42 pm

Umati wa wana-CUF walioandamana kumsindikiza Mgombea Urais, Prof. Ibrahim Lipumba, wakati aliporejesha fomu za uteuzi kwenye ofisi za Tume ya Uchaguzi ya Taifa, mjini Dar es Salaam. (Picha kwa hisani ya Muhiddin Issa Michuzi)

Imeandikwa na Waandishi Wetu

19th August 2010

Mkoani Kigoma, wanachama watano wa CCM walioshindwa kura za maoni wamekimbilia CUF.

Wanachama hao ni pamoja na aliyekuwa Kamanda wa Vijana wa CCM wa Wilaya ya Kigoma Vijijini, Optatus Likwelile, aliyejiunga na CUF na kuchukua fomu ya kuwania ubunge Kigoma Kusini.

Likwelile alishika nafasi ya tatu katika kura za maoni Kigoma Kusini akitanguliwa na Kiffu Hussein na mbunge aliyemaliza muda wake, Manju Msambya.

Kiffu ndiye mgombea wa CCM. Wengine waliochukua fomu ni Kiffu (CCM); David Kafulila (NCCR-Mageuzi); Muslim Hassanali (Chadema); Philip Fumbo (DP); Mvano Ramadhan (NRA); Zabibu Mrisho (UMD); Mwito Hailala (SAU); Aziza Hassan (Chausta); Selemen Msanu (Jahazi Asilia) na Mwajuma Malik (UPDP).

Mwingine aliyekimbia ni Omar Nkwarulo aliyejiunga na CUF na kuchukua fomu ya ubunge. Aligombea Kigoma Kaskazini, ambako alikuwa wa pili nyuma ya Lembo Robinson.

Jimbo hilo lilikuwa chini ya Zitto Kabwe wa Chadema anayewania tena kipindi cha pili. Msimamizi wa Uchaguzi wa majimbo hayo, Dominick Kweka alithibitisha wagombea hao kuchukua fomu. Wengine aliwataja kuwa ni Mfaume Mfaume (APPT-Maendeleo); Peter Mbolegwa (SAU); Tatu Hussein (UMD); Hamis Fadhil (NRA) na German Mlete (DP).

Aidha, Kweka alithibitisha kuwa jina la Sijapata Nkayamba aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), limepelekwa ofisini kwake na CUF akiwa mmoja wa wanaowania ubunge kupitia chama hicho.

Nkayamba aliwania ubunge Kigoma Kaskazini mwaka huu na katika kura za maoni za CCM, alishika nafasi ya tano, wakati mshindi akiwa ni Lembo.

Source: Habari Leo

 

Maalim Seif atangaza vipaumbele 10 vya Serikali ya Umoja wa Kitaifa atakayoiongoza

In Kiswahili on August 17, 2010 at 10:23 pm

Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, akipokea fomu za uteuzi kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Khatib Mwinchande jana tarehe 16 Agosti, 2010 huko ofisi za Tume hiyo, Maisara, mjini Zanzibar. (Picha kwa hisani ya Emmanuel Herman wa The Citizen/Mwananchi)

HOTUBA FUPI YA MAALIM SEIF SHARIF HAMAD KWA WAANDISHI WA HABARI BAADA YA KUCHUKUA FOMU ZA UTEUZI

Nimechukua fomu leo hii kutoka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ili niinue juu bendera ya CUF kwa madhumuni ya kuwaomba Wazanzibari ridhaa yao niweze kuiongoza Zanzibar Mpya tuliyoazimia kuijenga. Naamini tutafanikiwa. Lakini nilitaka basi niyataje japo kwa ufupi tu mambo kumi (10) ambayo yatakuwa ndiyo msingi wa maongozi yangu katika kipindi cha miaka mitano ijayo nitakapochaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, nikiwa naongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa, mambo ambayo yatakuwa ndiyo pia msingi wa Ilani ya Uchaguzi ya CUF kwa upande wa Zanzibar. Mambo hayo kumi (10) ni haya yafuatayo:

1. Kuyaendeleza Maridhiano ya Kisiasa tuliyoyaasisi mimi na Rais Amani Karume yakiwa ndiyo njia sahihi ya kujenga umoja wa kweli miongoni mwa Wazanzibari na kuendeleza amani na utulivu uliopo kwa kufuata misingi ya ukweli na mapatano. Katika hili, nitatekeleza matakwa ya Katiba ya Zanzibar kama ilivyorekebishwa hivi karibuni kwa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar.

2. Kuuimarisha Muungano wetu kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa kuendeleza mazungumzo yenye nia ya kweli ya kuyapatia ufumbuzi wa dhati matatizo yanayoukabili chini ya misingi ya haki, usawa na kuheshimiana baina ya pande mbili zinazounda Muungano huu.

3. Kujenga uchumi imara kwa kuzingatia mfumo wa soko huria unaotoa fursa ya ushiriki kwa wananchi wote na ambao unaratibiwa vyema na Serikali ili kuhakikisha kuwa wananchi wetu wote wanafaidika na fursa hizo na kunyanyua hali zao za maisha katika hali ya neema na tija kwa wote. Sekta za Kilimo, Uvuvi, Utalii, Biashara na Viwanda zitapewa kipaumbele katika ujenzi wa uchumi wa kisasa wa Zanzibar Mpya.

4. Kuimarisha nidhamu ya utendaji kazi Serikalini na ubora wa huduma zinazotolewa na utumishi wa umma kwa kusimamia ipasavyo kanuni za kazi, kuwapatia mafunzo ya kazi kadiri inavyowezekana na kuwaongezea mishahara wafanyakazi wetu ili wafanye kazi zao kwa ufanisi na kuwa mfano kwa umma.

5. Kwa kufuata mfumo wa uchumi wa soko huria, kuirudisha Zanzibar katika hadhi yake ya kituo kikuu cha biashara na huduma katika eneo lote la Afrika Mashariki kwa kutekeleza sera zitakazoweka mazingira mazuri na yanayovutia ya kufanyia biashara na kuleta uwekezaji mkubwa Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuimarisha bandari zetu na viwanja vya ndege vitakavyoweza kutuunganisha na nchi za nje na nchi jirani.

6. Kukiendeleza kilimo na kukirejeshea hadhi yake kama moja ya njia kuu za uchumi inayotegemewa na wananchi wetu walio wengi hasa wa vijijini. Mbali na mazao ya asili yaliyozoeleka, mkazo utawekwa katika kilimo cha viungo, mboga mboga na matunda ili tuendelee kutumia vyema soko linaloweza kupatikana kutokana na jina maarufu la Zanzibar kama visiwa vya viungo.

7. Kuimarisha miundo mbinu na sekta zinazohudumia za uchumi ikiwemo upatikanaji wa uhakika wa nishati ya umeme kwa kuongezea nguvu uzalishaji wa umeme wa dharura hapa hapa Zanzibar, kupatikana kwa huduma ya maji safi na salama, na ujenzi wa nyumba za kisasa na za gharama nafuu kwa watu wetu wote wa mijini na mashamba, na kupatikana kwa huduma za uhakika za usafiri wa nchi kavu, baharini na angani. Kipaumbele kitakuwa ni kuanzisha kwa Shirika la Ndege la Taifa la Zanzibar (Zanzibar Airways) ili kuiunganisha nchi yetu na maeneo muhimu ya kiuchumi na kibiashara duniani.

8. Kuweka msukumo maalum katika kuinua viwango vya elimu katika skuli zetu za msingi, sekondari hadi vyuo vikuu ili Zanzibar iwe ndiyo kituo kikuu cha elimu na mafunzo stadi katika eneo lote la Afrika Mashariki. Mkazo utawekwa katika kusomesha walimu kwa viwango vya kimataifa, kuwapatia maslahi bora ili kuirejeshea hadhi fani na kazi ya ualimu, kuboresha mazingira ya skuli zetu na taasisi za elimu ya juu kwa kuzipatia huduma zote muhimu zinazohitajika kwa ukuzaji wa elimu, kujenga na kuimarisha maabara za kisasa, kutilia mkazo teknolojia ya habari na mawasiliano (TEKNOHAMA), na kupunguza ukubwa wa madarasa na idadi ya wanafunzi ili walimu waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi na kuipitia upya mitaala yetu ili iendane na mahitaji ya Zanzibar ya leo kulingana na sera za uchumi tutakazozifuata.

9. Kuinua na kuimarisha huduma za afya katika hospitali, zahanati na vituo vya afya kwa kuweka vifaa vya kisasa vya matibabu, kuvipatia madawa yote muhimu, kusomesha na kuajiri madaktari na wauguzi wapya, kuboresha maslahi ya madaktari na wauguzi, kuwawekea mazingira bora ya kufanyia kazi na kuhakikisha usafi katika sehemu hizo.

10. Kurejesha maadili mema ya Wazanzibari kwa kuhuisha mila, silka na utamaduni wetu na kuwarejeshea Wazanzibari hadhi na fahari yao iliyotokana na mila, silka na utamaduni huo. Katika kurejesha maadili hayo, Serikali nitakayoiongoza itapambana vikali na uingizaji na utumiaji wa madawa ya kulevya ambao umekuwa ukiongezeka kwa kasi visiwani Zanzibar kwa kuhakikisha kuwa sheria zinatekelezwa na kusimamiwa ipasavyo ili kudhibiti uingizaji na pia kuanzisha na kuviendeleza vituo vya kuwasaidia waathirika wa madawa hayo ya kulevya ili waache utumiaji huo.

Haya niliyoyaeleza hapa siyo mambo pekee yatakayotekelezwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa nitakayoiongoza. Haya ni mambo nitakayoyapa umuhimu wa kipekee lakini yatajenga msingi wa kuyaendeleza mambo mengine katika sekta na nyanja zote za maisha. Haya na mengine yataelezwa na kufafanuliwa kwa upana zaidi katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama chetu tutakayoizindua wakati wa kampeni ukifika.

 

Seif Sharif Hamad

Zanzibar

16 Agosti, 2010

CUF yatangaza wagombea

In Kiswahili on August 9, 2010 at 11:49 am

CUF National Chairman, Prof. Ibrahim Lipumba, addressing a press conference at the party headquarters in ar es Salaam. Left is Director of Human Rights and Legal Affairs, Julius Mtatiro and right is Deputy Director for Information and Publi Relations, Ashura MUstapha.

Imeandikwa na Mwandishi Wetu

Tarehe: 7 August 2010

CHAMA Cha Wananchi (CUF), kimetangaza majina ya wagombea ubunge na uwakilishi kwenye uchaguzi mkuu ujao, huku aliyekuwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso), Julius Mtatiro akiteuliwa kuwania Jimbo la Ubungo, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, aliwambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kwamba baadhi ya majimbo ya Tanzania Bara na Zanzibar, mchakato wa kupata wagombea ubunge na uwakilishi unaendelea.

Profesa Lipumba aliwataja wagombea ubunge kwa Tanzania Bara na majimbo yao kwenye mabano kuwa ni Dar es Salaam, Hussein Siyovelwa (Ilala); Kimangale Mussa (Segerea); Heko Pori (Ukonga); Shaban Mapeyo (Kawe); Shabaan Nassor (Kinondoni) na Mustafa Mungwe (Kigamboni).

Tanga ni Mussa Mbarouk (Tanga Mjini); Remmy Shundi (Handeni); Bakar Mbega (Mkinga); Abubakar Bakari (Muheza); Gogola Gogola (Mlalo); Fabi Sozi (Bumbuli); Abassy Mkankamghanga (Lushoto), Jumaa Magogo (Korogwe Mjini); Mohamed Asiu (Korogwe Vijijini) na Omar Masomaso (Pangani).

Kilimanjaro ni Awadh Mwarabu (Same Magharibi). Mtwara ni Hassan Abdallah (Mtwara Mjini); Katani Katani (Tandahimba); Clara Mwatuka (Masasi); Mtikita Mtikita (Lulindi); Hakika Maarifa (Newala) na Chikamba Wanainuka (Mtwara Vijijini).

Lindi ni Salum Barwany (Lindi Mjini); Ayubu Nassor (Mchinga), Khalfan Mandanje (Mtama); Madaraka Beyi (Liwale), Nanjase Nanjase (Nachingwea), Abubakary Kondo (Ruangwa), Seleman Bungara (Kilwa Kusini) na Said Manoro (Kilwa Kaskazini).

Tabora ni Edward Zombwe (Urambo Mashariki), Kirungi Kirungi (Urambo Magharibi), Hassan Mwigwayasila (Igalula), David Kassoga (Tabora Kaskazini), Kidumla Kidumla (Bukene), Dominic Kizwalo (Nzega) na Abdallah Katala (Sikonge).

Kagera ni Christina Kasimbazi (Bukoba Vijijini), Nicolaus Batalingaya (Karagwe), Twaha Taslima (Bukoba Vijijini), Hamida Issa (Biharamulo Magharibi), David Tibanywana (Chato) na Yahya Ndyema (Nkenge).

Arusha ni Ghariby Baalawy (Arusha Mjini), John Pallangyo (Arumeru Mashariki), Adella Kileo (Arumeru Magharibi) na Navaya Ndaskoi (Monduli).

Mara ni Mustafa Wandwi (Musoma Mjini), Vedastus Msita (Mwibara) na Wilegi Songambele (Bunda).

Pwani ni Jafar Ndende (Mkuranga), Seif Porwe (Kibiti), Ali Kihambwe (Rufiji), Wahabi Twalut (Mafia), Adui Kondo (Kisarawe), Zahoro Vuai (Bagamoyo) na Miraj Mtibwiliko (Chalinze).

Shinyanga ni Mwalimu Mbukuzi (Shinyanga Mjini), Khanipha Ruhinda (Maswa Mashariki), Seif Baya (Maswa Magharibi), Jackson Deodatus (Bukombe), Shashu Lugeye (Solwa), Sauda Kasiga (Msalala), Hamisi Makapa (Kahama), Creoface Magere (Mbogwe) na James Matinde (Kisesa).

Kigoma ni Fatma Kinguti (Kigoma Mjini), Salum Kajanja (Buyungu), Athumani Hamisi (Muhambwe), Rashid Kaduguda (Kasulu Magharibi) na Ibrahim Magara (Buhigwe).

Mbeya ni Ezekia Mtafya (Ileje), Asukile Kabango (Mbozi Magharibi), Nkuyuntila Siwale (Mbozi Mashariki), Yusuf Said (Kyela) na Shaweji Salinyambo (Mbarali).

Iringa ni Mussa Fufumbe (Isimani), Godfrey Hongele (Njombe Kaskazini), Stanley Fwila (Njombe Kusini) na Jacob Mhanga (Njombe Magharibi).

Manyara ni Rashid Mgaya (Babati Mjini), Juma Nyeresa (Kiteto) na Eliseus Amedeus (Mbulu).

Ruvuma ni Mazee Mazee (Tunduru Kaskazini), Mohammed Mambo(Tunduru Kusini) na Hassan Mtwangambati (Namtumbo).

Morogoro ni Willy Dikundile (Kilosa Kati), Abeid Mlapakolo (Morogoro Mjini) na Blandina Mwasabwite (Morogoro Kusini Mashariki).

Mwanza ni Komanya Athanas (Buchosa), Mbaraka Chiru (Sengerema), Peter Malebo (Geita), Oscar Ndalahwa (Busanda), Andrea Mkanga (Nyang’hwale), Abdallah Mtina (Misungwi), Omar Mbalamwezi (Nyamagana), Mtebe Msita (Ukerewe), Ligawa Ndalahwa (Kwimba) na Julius Samamba (Sumve).

Katavi ni Aram Ndimubenya (Mpanda Mjini), Athumani Kababende (Mpanda Vijijini) na Abbas Ally (Katavi).

Singida ni Rashid Mindicar (Singida Mjini), Sizimwe Kanyota (Singida Kaskazini) na Dalfina Patric (Singida Magharibi).

Dodoma ni Ngomoka Joseph (Mtera), Ngomoka William (Chilonwa), Yahya Deni (Kondoa Kaskazini), Hassan Missanya (Kondoa Kusini). Tabora ni Kapasha Kapasha (Tabora Mjini).

Mwenyekiti wa CUF kwa Zanzibar aliwataja Faki Haji Makame (Mtoni), Rashid Soud Khamis (Bububu), Hassan Omar Issa (Mfenesini), Khamis Msabaha Mzee (Dole), Khatib Haji Ali (Fuoni), Ussi Juma Hassan (Mwanakwerekwe), Hamad Ali Hamad (Magogoni), Hemed Said Nassor (Dimani), Seif Suleiman Kombo (Amani) na Khamisi Ali Khamisi (Kwamtipura).

Wengine ni Ali Juma Khamisi (Chumbuni), Khamisi Mussa Haji (Kwahani), Idarous Habib Mohamed (Kikwajuni), Khalid Rajab Mghanah (Rahaleo), Suleiman Khamis Ally (Mpendae), Muhammad Ibrahim Sanya (Mji Mkongwe), Mohamed Yussuf Maalim (Jang’ombe) na Ahmed Khamis Hamad (Magomeni).

Aliwataja wengine kuwa ni Ramadhan Ali Mbarouk (Bumbwini), Ali Rashid Ali (Kitope), Othman Habibu Juma (Donge), Ali Mati Wadi (Matemwe), Yussuf Haji Khamis (Nungwi), Rashid Khamis Rashid (Tumbatu), Khamisi Suleiman Kombo (Chaani), Hassan Omar Nahodha (Mkwajuni), Abdi Mohamed Adeyoum (Uzini), Ali Khamis Ame (Chwaka) na Shabaan Iddi Ame (Koani).

Wamo pia Mohamed Kombo Ali (Makunduchi), Vuai Issa Haji (Muyuni), Mussa Haji Kombo (Chakechake), Ahmed Juma Ngwali (Ziwani), Hamad Rashid Mohammed (Wawi), na Haji Khatib Kai (Micheweni).

Wengine ni Rashid Ali Abdalla (Tumbe), Khatib Said Haji (Konde), Kombo Khamisi Kombo (Mgogoni), Mbaruk Salum Ali (Wete), Khalifa Suleiman Khalifa (Gando), Said Suleiman Said (Mtambwe), Rajab Mbarouk Mohamed (Ole), Rashid Ali Omar (Kojani), Salim Hemed Khamis (Chambani), Mohamed Habib Mnyaa (Mkanyageni), Masoud Abdalla Salim (Mtambile), Abdalla Haji Ali (Kiwani) na Ali Khamisi Seif(Mkoani).

Aidha, Profesa Lipumba aliwataja watakaowania uwakilishi katika Baraza la Wawakilishi kuwa ni Nassor Ahmed Mazrui (Mtoni), Bakar Haji Muhammad (Bububu), Masoud Nassor Seif (Mfenesini), Hasne Abdalla Abeid (Dole), Asha Ali Fakih (Fuoni), Idrisa Hamad (Mwanakwerekwe), Abdilah Jihad Hassan (Magogoni) na Manzi Ibrahim Juma (Kiembesamaki).

Wengine ni Ali Juma Ali (Dimani), Khamis Rashid Abeid (Amani), Dk. Majaliwa Juma Seif (Kwamtipura), Maulid Suleiman Juma (Chumbuni), Hassan Juma Hassan (Kwahani) na Bakar Hassan Bark (Kikwajuni).

Wengine ni Omar Mussa Makame (Rahaleo), Maharouk Abdalla Suleiman (Mpendae), Ismail Jussa Ladhu (Mji Mkongwe), Haji Ameir Muhunzi (Jang’ombe), Zainab Omar Mzee (Magomeni), Zahran Juma Mshamba (Bumbwini), Hassan Khatib Kheri (Kitope), Machano Omar Masanja (Donge) na Shauri Makame Mkadam (Matemwe).

Wagombea uwakilishi wengine ni Haji Mwadini Makame (Nungwi), Makame Hamad Makame (Tumbatu), Khamis Amour Vuai (Chaani), Vuai Kona Haji (Mkwajuni), Salma Hussein Zaral (Uzini), Ali Mrisho Haji (Chwaka), Khamis Malik Khamis (Koani) na Ameir Mussa Ameir (Makunduchi).

Wengine ni Suleiman Hassan Suha (Muyuni), Omar Ali Shehe (Chakechake), Rashid Seif Suleiman (Ziwani), Saleh Nassor Juma (Wawi), Abdalla Juma Abdalla (Chonga), Subeti Khamis Faki (Michweweni), Rufai Said Rufai (Tumbe), Suleiman Hemed Khamis (Konde), Abubakar Khamis Bakary (Mgogoni) na Asaa Othman Hamad (Wete).

Wagombea wengine ni Said Ali Mbarouk (Gando), Salim Abdalla Hamad (Mtambwe), Hamad Masoud Hamad (Ole), Omar Ally Jadi (Kojani), Mohammed Mbwana Hamad (Chambani), Haji Faki Shaali (Mkanyageni), Muhamed Haji Khalid (Mtambile), Haji Hassan Hija (Kiwani) na Abdalla Mohamed Ali (Mkoani).

Kuhusu utaratibu wa kupata wagombea hao, Lipumba alisema kwa Zanzibar mchakato ulifanyika matawini kama ilivyofanya CCM kutokana na jiografia, lakini kwa Bara ilishindikana kutokana na ukubwa wa maeneo.

Alisema kutokana na kushindwa kufikia kila sehemu, wagombea walituma maombi ambayo yalijadiliwa na mkutano mkuu kabla ya kupelekwa Baraza Kuu la Chama kuteuliwa.

CUF ambacho ni chama kikuu cha upinzani Zanzibar, kinakuwa cha kwanza kukamilisha uteuzi wa wagombea wake wa ubunge na uwakilishi, kwani vyama vingine vinaendelea na mchakato.

CCM iliendesha kura za maoni za uteuzi Agosti mosi mwaka huu na sasa vikao vya uteuzi kwa ngazi ya wilaya na mikoa vinaendelea kabla ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kukutana Agosti 15 mwaka huu Dodoma kufanya uteuzi wake.

Chanzo: HabariLeo

 

Uongozi na Uadilifu katika Siasa

In Kiswahili on July 13, 2010 at 1:57 pm

 

Na Ismail Jussa*

__________________________________________

 

Politics is a dirty game

Siasa ni mchezo mchafu

 

Politics is a game of perception

Siasa ni mchezo wa hisia

 

Politics is the art of the possible

Siasa ni sanaa ya yanayomkinika

 

Politics is an art of compromise

Siasa ni sanaa ya suluhu

 

Power tends to corrupt and absolute power corrupts absolutely

Madaraka hufisidi na madaraka yasiyo na kikomo hufisidi bila ya kikomo

 

 

UTANGULIZI

 

Nukuu hizo hapo juu zinatosha kuonesha kuwa kuzungumzia uongozi na uadilifu katika siasa si jambo jepesi. Hisia na mitazamo ya watu wa kawaida kuhusiana na ‘siasa’ imekuwa ya kuihusisha fani hiyo na tamaa, ubinafsi, uroho, unafiki, ulaghai, upotovu, uovu, fitina, khiyana, na hata hujuma. Tena si watu wa kawaida tu bali hata baadhi ya wasomi wetu wanaonekana kuiona hivyo. Katika makala yake, ‘Kuuawa kwa Rais Abeid Amani Karume: Ni Mapinduzi au Chuki Binafsi?’, iliyochapishwa kwenye gazeti la Rai la Mei 2430, 2007, mwandishi Joseph Mihangwa aliandika kuwa, “Siasa ni mchezo mchafu” na “siasa si hasa.” Kwa mantiki hii, katika siasa hakuna udugu wala urafiki, na kama upo basi huwa ni wa muda tu.”

Tulipokuwa tunasomeshwa siasa (sasa Civics au Uraia) maskulini tukifundishwa kuwa, “Siasa ni fikra, busara na mipango ya kuongoza na kuendesha nchi.” Basi kipi tena kilichowafanya Watanzania kuipa siasa kila sifa mbaya na kuiita majina yasiyopendeza? Je, kuna tatizo katika siasa yenyewe au ni ‘wanasiasa’ ndiyo wenye matatizo kiasi cha kufikia kuitukanisha fani hii muhimu katika maisha ya kila siku ya mwanadamu. Niliwahi kusoma mahojiano katika gazeti moja (ingawa sikumbuki ni lipi) na mwanasiasa mkongwe na maarufu wa Zanzibar, Dk. Salim Ahmed Salim, ambapo alitetea kwa nguvu zote kuwa “Siasa si mchezo mchafu, ila wachezaji wake ndiyo wachafu.”

Ni madhumuni ya waraka huu kujaribu kuonesha nini inapaswa kuwa misingi ya siasa, siasa husarifiwa na nini na yenyewe husarifu nini, kuna mahusiano gani kati ya waongozi na waongozwa, sifa na vigezo vya kiongozi wa siasa, uadilifu kama msingi wa maongozi ya nchi, uzoefu wa Zanzibar katika uongozi na uadilifu katika siasa, athari za kukosekana uadilifu katika uongozi wa kisiasa, iwapo kweli kunaweza kukawepo na uadilifu katika siasa, na mwisho nini kifanyike kurejesha uadilifu katika siasa.

 

MISINGI YA SIASA KATIKA MAONGOZI YA NCHI

Msingi wa siasa ni utumishi kwa umma. Ni fani inayohusu uendeshaji wa jamii, nchi au taifa. Katika dhana ya kisasa, ambapo wananchi kutokana na wingi wao waliridhika kuwa wasingeweza kwa pamoja kukutana, kufanya maamuzi na kuyasimamia moja kwa moja maamuzi hayo yanayowahusu wao kama jamii, ilionekana haja ya kuwa na taasisi ambazo zingepewa majukumu ya kusimamia na kuongoza nyanja tofauti za maisha yao. Taasisi hizo, katika mfumo wa maongozi ya nchi kwa njia za kidemokrasia, hupewa ridhaa (mandate) na wananchi kupitia maamuzi yao ya pamoja (kwa njia ya kura). Hiki kilikuwa ndiyo chanzo cha kuwa na kanuni zinazotawala maisha ya jamii, kwa raia mmoja mmoja na kwa jamii kwa pamoja. Ilibidi ziwepo haki za binadamu na za raia ambazo jamii ilipaswa kumhakikishia kila mtu na na pia kutambuliwe wajibu ambao kila mtu anapaswa kuuheshimu na kuutekeleza kwa jamii yake. Na katika kuyasimamia na kuyahakikisha yote hayo, ndipo dhana ya kuwepo Serikali katika hatua za awali na baadaye Mamlaka ya Kutunga Sheria na Mahkama ilibuniwa zikiwa ndiyo mamlaka zenye dhima hiyo. Utaratibu, nidhamu, mipango na busara ya kuyapata yote hayo, utekelezaji wake, na usimamizi wake ndiyo huitwa siasa. Ndiyo maana halisi ya Siasa kufasiriwa kuwa ni fikra, busara na mipango ya kuendesha nchi

Kwa mukhtasari huo, itaonekana tokea mwanzo kuwa siasa ni nguvu (power), na nguvu hiyo ni nguvu ya pamoja inayowakilisha jamii ambayo hupatikana kutokana na kule kuchangiwa kwake na nguvu za kila mmoja katika jamii hiyo. Serikali hupata uhalali wa kutawala kutokana na kuchangiwa na nguvu hiyo. Mamlaka ya Kutunga Sheria hupata uhalali wa kutunga Katiba, Sheria na Kanuni zinazoongoza maisha yetu ya kila siku kutokana na kuchangiwa na nguvu hiyo. Na Mahkama nayo hupata uhalali wa kusimamia utekelezaji wa katiba, sheria na kanuni hizo na kusimamia utoaji wa haki kutokana na mamlaka wanayopewa na ama Mkuu wa Serikali au Mamlaka ya Kutunga Sheria ambao nao wamepewa nguvu na wananchi.

Wale Wakuu wanaosimamia mambo yetu, wawe katika Serikali, Mamlaka ya Kutunga Sheria au Mahkama au wawe katika taasisi zinazotumika kuyafikia mamlaka hayo ikiwa ni pamoja na vyama vya siasa, ndiyo wanaosimamia na kuongoza kila ncha inayogusa maisha yetu ya kila siku, iwe ni katika utawala na uendeshaji wa nchi, haki na wajibu wetu, harakati za uchumi na kujitafutia riziki, na utoaji wa huduma za jamii. Hayo ni mamlaka makubwa ambayo yanaambatana na nguvu kubwa.

Mpaka hapo itaonekana kuwa kusudio la siasa ni jema, na si hasha takatifu na adhimu kabisa, lililojikita katika dhana safi ya utumishi wa umma. Hiyo ni sahihi unapotazama upande mmoja wa sarafu lakini kutokana na maumbile yake, kutokana na nguvu zinazoambatana nayo, basi siasa pia katika upande wa pili wa sarafu inamaanisha ulwa (madaraka), fursa na ushawishi (influence) mkubwa katika jamii, na mambo hayo yakitumiwa vibaya pia yanazaa utajiri ambao mara nyingi unakuwa si wa halali.

Ulwa (madaraka), fursa na ushawishi katika jamii huweza kutumiwa vizuri kwa maslahi ya jamii lakini vina kawaida pia ya kumpa kiburi cha namna fulani mwenye navyo na asipowekewa vikomo (limits) kwa njia ya vizuizi na mizania (checks and balances) basi kuna hatari ya ‘kulewa’ navyo na kuvitumia kuifisidi jamii. Ni katika muktadha kama huo, ndipo Lord Acton akasema kuwa “Power tends to corrupt and absolute power corrupts absolutely” yaani madaraka hufisidi na madaraka yasiyo na kikomo hufisidi bila ya kikomo.

Huko nyuma katika historia Serikali (Mamlaka ya Utawala) ilikuwa katika mfumo wa Ufalme na Mfalme alikuwa na mamlaka yote (Sovereign) ya kuwahukumu raia wake apendavyo, mamlaka ambayo yakiaminiwa kuwa yanatokana na Mwenyezi Mungu. Zama hizo zilikuwa za tawala ambazo raia hakuwa na haki ya kuhoji lolote. Unahoji kitu gani ikiwa mamlaka imetoka kwa Mungu mwenyewe? Mapambano ya muda mrefu katika jamii ndiyo hatimaye yakapelekea kuwepo kwa Mamlaka ya Kutunga Sheria, ikiwa na mfumo wa katiba na sheria katika nchi, ili kudhibiti nguvu za Mtawala kufanya atakavyo. Kidogo kidogo mamlaka ya kutawala yaliondoka katika dhana ya Ufalme unaopata uhalali kutokana na ‘kudura’ ya Mwenyezi Mungu na kuja katika Serikali zinazochaguliwa ambazo hupata uhalali kutoka kwa wananchi wenyewe wanaopiga kura kuziweka na kuziondoa madarakani.

Kwa kiasi kikubwa hizi ndiyo aina ya tawala ambazo ziko ulimwenguni hivi sasa zikiwa ama katika mfumo wa kuwa na Mfalme wa Kikatiba (Constitutional Monarchy) akiwa Mkuu wa Nchi na Waziri Mkuu akiwa Mkuu wa Serikali kama ilivyo kwa nchi za Uingereza, Canada, Australia, Denmark, Norway, Sweden, Uholanzi, Japan, Thailand, Morocco, na Lesotho au mfumo wa Jamhuri (Republic) ambao nao umegawika kati ya ule unaoongozwa na Rais asiye na madaraka (Ceremonial President) akiwa Mkuu wa Nchi na Waziri Mkuu akiwa Mkuu wa Serikali kama ilivyo katika nchi za India, Ujerumani, na Malaysia, na ule unaoongozwa na Rais mwenye madaraka akiwa Mkuu wa Nchi na Serikali (Executive President) ambaye hutekeleza majukumu yake kwa kusaidiana na Waziri Mkuu (au katika nchi nyengine Makamu wa Rais) kama vile ilivyo katika Marekani, Ufaransa, Finland, Urusi, Brazil, Argentina, Pakistan, Sri Lanka, Indonesia, Korea Kusini, Afrika Kusini, Kenya, Uganda, Tanzania, na hata Zanzibar.

 

MAHUSIANO YA WAONGOZI NA WAONGOZWA KATIKA SIASA

Kama ilivyoelezwa kabla, msingi mzima wa siasa katika maongozi ya tawala za kidemokrasia (na hata baadhi ya tawala za kidikteta hudai hivyo hivyo) unahusu ridhaa (mandate) ambayo wanaoongozwa huitoa kwa waongozi na hivyo kuwapa uhalali wa kusimamia mambo yao. Lakini ridhaa hiyo haitolewi hivi hivi tu, inaambatana na amana (trust) kwamba waongozi watatekeleza dhamana (obligations) na wajibu (duties) wao kwa makubaliano na maelewano ya kufuata barabara na kuheshimu ipasavyo kanuni na maadili (norms, values and tastes) fulani yanayoitambulisha na kuiongoza jamii husika. Marcus Tullius Cicero katika kitabu chake cha The Republic, kama kilivyonukuliwa na Chris Paten kwenye kitabu chake, East and West, Uk. 146 anayaeleza mahusiano haya kama ifuatavyo:

“Well, then, a commonwealth is the property of a people. But a people is not any collection of human beings brought together in any sort of way, but an assemblage of people in large numbers associated in an agreement with respect to justice and a partnership for the common good. The first cause of such an association is not so much the weakness of the individual as a certain social spirit which nature has implanted in man.”

Katika mifumo ya kileo, mambo haya huwekwa katika katiba na sheria za nchi ambazo zinajumuisha misingi ya jumla ya maongozi ya nchi, na pia huwekwa katika ilani (manifesto) za uchaguzi ambazo vyama vya siasa huziwasilisha kwa wapiga kura ili kupata ridhaa yao katika kuamua sera zitakazofuatwa na Serikali katika kipindi maalum kilichowekwa (hapa kwetu ni miaka mitano) baada ya uchaguzi kukamilika. Vitu hivyo viwili – Katiba na Ilani – huwa ndiyo mkataba baina ya waongozi na waongozwa katika uendeshaji wa nchi na Serikali.

Dhana ya demokrasia ambayo ilianzishwa na Wagiriki na sasa inabeba misingi ya kileo ya maongozi ya nchi inasisitiza suala hilo la mapatano yanayoongoza nchi baina ya waongozi na waongozwa. John Uhr katika kijitabu chake, Creating a Culture of Integrity, ameifafanua vyema tafsiri hii ya demokrasia pale aliposema:

“Democracy at its simplest refers to government by the people, carried out in the interests of the whole community. Democracy is often called ‘people power’. The central democratic idea is popular sovereignty: the idea that the people are the ultimate sovereign and that ‘good government’ demands that those who govern do so as representatives of the people whose welfare they hold in trust. Popular sovereignty is translated into practice by the people’s right to vote, and to stand for office, and so determine who governs. The legitimacy of democratic governments flows from their dependence on the freely-expressed consent of their citizens. Elections provide one important opportunity for the expression of popular consent. Elections also serve an important accountability function by reminding those who govern that they are meant to put the public good ahead of their own particular interests. Elections are thus important tests of accountability for governments as well as tests of popular consent to either the serving government or to alternative parties or individuals seeking a representative role.”

Ndiyo maana wanafalsafa huiita Katiba kuwa ni mkataba kati ya watawala na watawaliwa. Kwa maneno mengine, ni mkataba wa amana (trust) ambao unaongoza mahusiano kati ya waongozi na waongozwa. Wakati mwengine mahusiano haya pia huja katika mfumo wa Mkataba wa Kijamii (Social Contract) kama ilivyokuwa Ufaransa baada ya Mapinduzi ambao uliweka misingi ya Uhuru, Usawa na Udugu (Liberty, Equality and Fraternity).

Katika katiba, msingi wa mahusiano hayo ya waongozi na waongozwa huwekwa katika Utangulizi (Preamble). Kwa mfano, Utangulizi wa Katiba ya Zanzibar unaeleza nia ya wenye katiba (sponsors of this constitution) ambao ni wananchi juu ya vipi Zanzibar iongozwe. Hivyo madaraka liliyo nayo Baraza la Wawakilishi, ambalo ndilo lililotunga katiba hiyo mwaka 1984, yanatokana na wananchi na kwamba Baraza linayashikilia madaraka hayo kama amana (trust) kwa niaba ya wananchi hao. Sehemu ya utangulizi huo inabainisha:

“NA KWA KUWA SISI, Wananchi wa Zanzibar tumeamua rasmi na kwa dhati kujenga katika nchi yetu jamii inayozingatia misingi ya uhuru, haki, udugu na amani;

NA KWA KUWA misingi hiyo yaweza tu kutekelezwa katika jamii yenye demokrasia ambayo Serikali yake husimamiwa na Baraza la Wawakilishi lenye wajumbe waliochaguliwa na linalowakilisha wananchi, na pia yenye Mahkama huru zinazotekeleza wajibu wa kutoa haki bila woga wala upendeleo wowote, na hivyo kuhakikisha kwamba haki zote za binadamu zinadumishwa na kulindwa na wajibu wa kila mtu unatekelezwa kwa ukamilifu;

KWA HIYO BASI, KATIBA HII IMETUNGWA NA BARAZA LA WAWAKILISHI KATIKA KIKAO CHAKE cha tarehe 9 Oktoba, 1984 kwa niaba ya Wananchi, kwa madhumuni ya kujenga jamii kama hiyo, na pia kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Zanzibar inaongozwa na Serikali yenye kufuata misingi ya demokrasia na ya kijamaa.”

Kwa hiyo, kushindwa kwa Serikali kusimamia misingi ya katiba ni sawa na kwenda kinyume na amana waliyokabidhiwa na watu wa Zanzibar.

Isitoshe, vifungu vya Katiba yenyewe vinaeleza kuwa mamlaka ni ya wananchi. Haya yanaelezwa wazi katika kifungu cha 9 cha Katiba ya Zanzibar kinachosema:

“9.-(1) Zanzibar itakuwa ni nchi ya kidemokrasia na haki za kijamii.

       (2) Kwa hiyo hapa inaelezwa rasmi kwamba:

(a) Mamlaka ya kuendesha nchi ni ya wananchi wenyewe ambapo nguvu na uwezo wote wa Serikali kufuatana na Katiba utatoka kwa wananchi wenyewe.”

Kwa vile Zanzibar ni Jamhuri inayoongozwa na rais mwenye madaraka (executive president) hivyo basi Rais wa Zanzibar ndiye mlinzi wa dhamana (custodian) wa mamlaka ya watu wa Zanzibar, na anapaswa kuchukua jukumu la mbele (vital role) katika kuhakikisha kuwa Wazanzibari wanaongozwa kwa uadilifu kufuatana na mkataba uliowekwa ambao ni Katiba ya Zanzibar. Na wananchi nao wana dhamana ya kwanza kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kama raia na pia wanatetea na kuzilinda haki zao na za raia wenzao ili uadilifu kati ya waongozi na waongozwa usimame juu ya msingi imara.

 

UADILIFU WA UONGOZI KATIKA SIASA NI UPI?

Mtu angeweza kusema kuwa maelezo yaliyotangulia hayatoi nafasi ya kuwepo uadilifu wa uongozi katika siasa kwa sababu ya maumbile yake. Mtu anapotazama maisha ya kila siku ya wanasiasa ataiona siasa imejikita katika kukimbilia na kupigania ulwa, fursa na ushawishi kwa malengo ya kujilimbikizia uwezo wa maamuzi na wa utajiri binafsi usiohojiwa kuliko kuzingatia kwamba siasa ni utumishi wa dhati na uliotukuka kwa umma uliozindukana. Huo ni udhaifu wa mwanadamu ambao hapaswi kuupa nafasi iwapo anazingatia uadilifu wa uongozi. Mwanafalsafa maarufu wa Kichina, Confucius, anatwambia katika The Analects of Confucius, 4.5:

‘The Master said: ‘Riches and rank are what every man craves; yet if the only way to obtain them goes against his principles, he should desist from such a pursuit.’

‘Utajiri na vyeo ndivyo vitu ambavyo kila bianadamu anavitamani; lakini ikiwa njia ya kuvipata ni kwa kwenda kinyume na misingi yake, anapaswa ajiepushe navyo.’

Hata hivyo, si sahihi wala si haki kudhani kwamba siasa hutumiwa kwa malengo ya kutimiza haja binafsi kama hizo tu.

Siasa bado imebaki kuwa fani muhimu ya kuwatumikia wananchi na ina misingi na maadili yake kama zilivyo fani nyengine. Iwapo wachezaji (iwe wengi au wachache) hawaheshimu misingi na maadili hayo, tatizo litakuwa ni la wanasiasa na siyo la siasa. Mmojawapo wa wasomi wanaoheshimika hapa Tanzania, Profesa Issa Shivji, aliwahi kuiambia Tume ya Nyalali mwaka 1991 kuwa, “Wanafalsafa wanapenda siasa lakini hawapendi madaraka, wanasiasa hawapendi siasa, wanapenda madaraka.” Lakini basi ni yepi hayo maadili ya uongozi wa kisiasa?

Si rahisi kuchukua nadharia moja ukaitumia kuweka maadili ya uongozi wa kisiasa lakini waraka huu ukisaidiwa na maandiko mbali mbali ya wanafalsafa na wachambuzi wa masuala ya siasa unapendekeza kutafakari kwa pamoja vigezo vifuatavyo vya kiongozi muadilifu katika siasa.

 • Kiongozi anaongoza, haongozwi

Kwa mtazamo wangu, msingi wa kwanza wa uadilifu wa uongozi katika siasa unapaswa uwe ule uliomo katika neno lenyewe “kiongozi” kwa maana ya kuonesha njia. Msingi huu unaaminisha kuwa kiongozi kwanza awe muadilifu kwa uongozi wake na hivyo awe anaongoza badala ya kuongozwa. Kiongozi katika jamii anatakiwa awe ametambuliwa na kukubalika na wanajamii kutokana na sifa fulani alizo nazo zinazomtofautisha na wengine na hivyo kuaminika kuwa anaweza kuonesha njia kwa wale wanaomuona ana uwezo huo. Uongozi kama huu mara nyingi huambatana na mvuto wa maumbile (charisma) inayowapelekea wanajamii kwa hiyari zao wenyewe kujikubalisha na kutoa utiifu wao kwa yule wanayemuona kiongozi wao. Kiongozi wa aina hii huwa na kipawa na kipaji fulani kinachompa nafasi ya kuona zaidi kuliko wengine lakini pia akitumia habari na taarifa ambazo wengine hawazipati kuweza kufikia maamuzi yenye maslahi na jamii nzima. Rudolph Giuliani, aliyekuwa Meya wa New York wakati wa matukio ya Septemba 11, akiandika kuhusu Uongozi kwenye kitabu chake, ‘Leadership’, Uk. 207 anasema:

“A leader is chosen because whoever put him there trusts his judgment, character, and intelligence – not his poll-taking skills. It’s a leader’s duty to act on those attributes.”

‘Kiongozi huchaguliwa kwa kuwa yeyote anayemuweka pale huwa anaamini maamuzi, tabia na uwezo wa maarifa yake – siyo ujuzi wa kufuata maoni. Ni wajibu wa kiongozi kuchukua hatua kufuatana na sifa hizo.’

Kwa nafasi hiyo, kiongozi muadilifu hakubali kufuata upepo wa maoni ya jamii tu (opinion polls) ambayo huyumba kulingana na wakati na mara nyingi hayazingatii maslahi ya muda mrefu. Kiongozi anayesikiliza mdundo na kisha kufanya maamuzi yake kulingana na ‘mdundo’ uendavyo (populist) huwa amekimbia dhamana kuu ya uongozi na huishia kuyumba na kuiyumbisha jamii anayoiongoza. Kusema hivi hakuna maana ya kiongozi kuwa dikteta na kutosikiliza maoni ya anaowaongoza. La hasha! Maoni na ushauri ni muhimu, lakini hayo hayondoshi dhamana ya kiongozi kutumia kipaji, kipawa, taarifa na busara za uongozi kufanya maamuzi na kuyasimamia. Confucius anatwambia katika The Analects of Confucius, 2.24:

‘The Master said: ‘To worship gods that are not yours, that is toadyism. Not to act when justice commands, that is cowardice.’

‘Kuabudu miungu isiyo yako, huko ni kujikomba. Kutochukua hatua pale uadilifu unapokutaka ufanye hivyo, huo ni woga.’

 • Kiongozi anapaswa azingatie maslahi ya nchi na watu wake hata kama watu wataona anayoyafanya hayana maslahi nao kutokana na ufinyu wa taarifa

Uwezo na madaraka huambatana na dhamana (power comes with responsibility). Hivyo, dhana ya kiongozi kuongoza badala ya kuongozwa inaambatana pia na dhamana ya kuhakikisha na kujiridhisha kuwa mara zote maamuzi anayoyatoa na kuyasimamia yamefanywa kwa maslahi ya nchi na watu wake. Mara nyengine hali hii huambatana na wale anaowaongoza kuona kuwa maamuzi hayo si sahihi na hayana maslahi nao lakini hayo huweza kusababishwa na waongozwa kutokuwa na taarifa ambazo kiongozi kwa nafasi yake huwa nazo. Hivyo, unabaki kuwa wajibu muhimu wa uadilifu wa uongozi katika siasa kuwa kila maamuzi yanayofanywa yawe yametokana na kujiridhisha kwa kiongozi huyo kuwa yanawakilisha maslahi bora zaidi kwa anaowaongoza. Yanaweza kuwa na athari za muda mfupi na mara nyengine kuwa na machungu lakini alimradi tu machungu hayo ni ya muda mfupi, uadilifu wa uongozi unadai kiongozi kutoyumba wala kutetereka katika kuyatetea.

 • Kiongozi anatakiwa awe mfano kwa anaowaongoza

Kuweza kuyafanikisha mambo hayo mawili yaliyotajwa hapo juu, kiongozi anapaswa kuwa mfano bora kwa anaowaongoza kwa kuwa na ‘moral command’ ambayo huja kwa yeye mwenyewe kuyafuata na kuonekana anayafuata yale anayoyadai kutoka kwa anaowaongoza. Kwa maneno mengine, kiongozi anatakiwa atembee juu ya maneno yake (A leader has to walk his talk). Kwa mfano, huwezi ukawataka raia wafuate sheria wakati wewe mwenyewe unaongoza kwa kuvunja sheria, huwezi kuwataka raia wasijiingizie katika rushwa wakati wewe unakula na kunywa, unalala na kuamka na rushwa. Huwezi kuwaambia raia wapambane wakati wewe unakimbia vita. Confucius anasema katika The Analects of Confucius, 14.27 kwamba ‘A gentleman would be ashamed should his deeds not match his words’ yaani muungwana anapaswa kuona aibu iwapo vitendo vyake havilingani na kauli zake.

 • Kiongozi anapaswa azingatie haki na uadilifu kwa anaowaongoza (wanaomkubali na wasiomkubali)

Msingi wa uongozi ni uadilifu. Kiongozi anapaswa kusimamia haki na uadilifu kwa wote anaowaongoza bila ya upendeleo wala chuki.  Haki na uadilifu huu uonekane katika usawa mbele ya sheria, kufaidi fursa za nchi kwa usawa, na kuwepo kwa urari wa maendeleo kati ya sehemu zote za nchi. Isitokee sehemu ya jamii au nchi ikahisi inatengwa, kudharauliwa, kubaguliwa, kunyanyaswa au kukandamizwa. Watu wote wajione wana haki na fursa sawa. Waongozwa wakiona hayo na kuridhika, utiifu wao kwa waongozi huwa hauna shaka, na hutokana na hiyari ya kweli. Na kama wasemavyo wahenga, hiyari yashinda utumwa.

 • Kiongozi azingatie umoja wa anaowaongoza

Kiongozi muadilifu mara zote atahakikisha kunakuwepo umoja miongoni mwa anaowaongoza kwani huwa anauhitaji umoja huo kushajiisha na kuchechemua maendeleo ya nchi na watu wake. Kiongozi muadilifu hawagawi anaowaongoza kwa kuwa hana sababu ya kufanya hivyo. Kwa hakika umoja wa Taifa analoliongoza ni fakhari ya kiongozi muadilifu. Kiongozi anayewagawa watu ni muovu, huwa hawaamini anaowaongoza na huwaogopa. Ili kujihami yeye na madaraka aliyo nayo, kiongozi muovu huishia kuwagawa watu wake kwa kupandikiza chuki na fitina. Isitoshe, mara nyingi misingi ya umoja katika nchi humong’onyoka ikiwa ni matokeo ya kiongozi kushindwa kusimamia haki na uadilifu.

 • Kiongozi azingatie amani na utulivu katika nchi

Kama ilivyo kwa umoja wa kitaifa, kiongozi muadilifu pia hufanya kila bidii kuhakikisha amani na utulivu wa kweli katika nchi vinapatikana. Amani na utulivu ni chachu ya wananchi kwa kushirikiana na Serikali yao kujiletea maendeleo. Maendeleo hayaji mahala penye magomvi na hasama. Lakini na amani na utulivu pia haviji mahala pasipo na haki na uadilifu. Uvunjifu wa amani na utulivu wa nchi hupelekea hasara ya maisha na mali ya watu na hayo hayawi malengo ya uongozi muadilifu katika nchi.

 • Kiongozi asikubali kuona ukandamizaji wa aina yoyote

Yaliyotajwa hapo juu – haki, uadilifu, umoja, amani na utulivu – yanapatikana pale ambapo hakuna ukandamizaji wa aina yoyote dhidi ya raia. Uadilifu wa uongozi katika siasa unadai kiongozi kuchukua hatua za makusudi, za dharura na za haraka kuondosha ukandamizaji wa aina yoyote ile iwapo utathibitika au hata kudhaniwa tu. Wanasayansi wa siasa wanasema siasa ni mchezo wa dhana au hisia (politics is a game of perception). Kwa hivyo haki inapaswa sio tu itendeke bali ionekane kuwa inatendeka ili kuodosha uwezekano, hata kama ni mdogo kiasi gani, wa kuhisiwa kuwepo na ukandamizaji dhidi ya wengine. Kwa kuazima tena falsafa za Confucius kutoka kwenye The Analects of Confucius, 15.24, anasema:

‘Zigong asked: ‘Is there any single word that could guide one’s entire life?’ The Master said: ‘Should it not be reciprocity? What you do not wish for yourself, do not do to others.’

‘Zigong aliuliza: ‘Je, kuna neno moja tu linaloweza kumuongoza mtu maisha yake yote?’ Mwalimu akasema: ‘Lisiwe ni marejesho? Yaani kile usichokipendelea nafsi yako, usiwafanyie wengine.’

 • Kiongozi awe muumini wa kweli wa demokrasia

Jamii siku zote haiachi kuwa na mgongano wa fikra, na mgongano huu ni muhimu na unahitajika katika kuipeleka jamii hiyo mbele. Fikra zinapogongana na kushindanishwa hupelekea hoja madhubuti kuibuka na hivyo maamuzi kufikiwa kwa kuzingatia nguvu ya hoja na fikra bora. Uadilifu wa uongozi unadai kuheshimu nguvu ya hoja na fikra bora na hayo yanaweza kupatikana tu iwapo nchi inaongozwa kwa misingi ya kidemokrasia. Hivyo, katika kutoa uongozi sahihi, kwa kuzingatia maslahi bora ya nchi na watu wake, haki, uadilifu, umoja, amani na utulivu, hapana budi kwa kiongozi kuiamini, kuiheshimu na kuifuata barabara misingi ya kidemokrasia. Kwa maneno ya Confucius tena kutoka The Analects of Confucius, 13.15:

‘Is there one single maxim that could ruin a country?’

Confucius replied: ‘Mere words could not achieve this. There is this saying, however: “The only pleasure of being a prince is never having to suffer contradiction.” If you are right and no one contradicts you, that’s fine; but if you are wrong and no one contradicts you – is this not almost a case of “one single maxim that could ruin a country”?’

‘Je, kuna methali moja tu inayoweza kuifisidi nchi?’

Confucius alijibu: ‘Maneno matupu hayawezi kulifanikisha hilo. Uko usemi huu, hata hivyo: “Furaha pekee ya kuwa mwana mfalme ni kutopingwa.” Ikiwa utakuwa sahihi na hakuna anayekupinga, hiyo ni sawa; lakini ukiwa makosani na hakuna anayekupinga – je, hii haiwi aina ya “methali moja tu inayoweza kuifisidi nchi”?’

 • Kiongozi anapaswa kuwajibika kwa yanayotendwa kwa jina lake

Pamoja na kuzingatia yote yaliyotajwa hapo juu, bado binadamu si mkamilifu na kwa vyovyote vile hufikia mahala akafanya maamuzi ambayo si sahihi hata kama yalifanywa kwa nia njema na kwa kuzingatia taarifa zilizopatikana wakati maamuzi hayo yanafanywa. Hayo yanaeleweka na kiongozi muadilifu anapaswa kuyakubali. Hata hivyo, inapotokezea maamuzi yanayofanywa na dola au taasisi yoyote yakaleta madhara au yakasababisha kuchafua jina jema la wadhifa ambao kiongozi wa kisiasa anaushikilia, basi uadilifu wa uongozi unamtaka yule aliyesababisha hayo au ambaye maamuzi yanayohusika yalifanywa kwa jina lake awajibike. Kwa mtazamo wangu, hiki ndiyo kilele na kigezo kikuu cha uadilifu wa uongozi katika siasa. Kukubali kubeba dhamana kwa madhara yaliyotokana na maamuzi yako au yaliyofanywa kwa jina lako.

 • Kiongozi awapende anaowaongoza

Itadhihirika mpaka sasa kwamba dhima anazotwishwa nazo kiongozi wa siasa ni kubwa na zinahitaji uimara wa nafsi katika kuzisimamia. Yote yanayofanywa hufanywa kwa jina la watu (in the name of the people). Imeonekana kwa mfano, mara nyengine kiongozi hulazimika kufanya maamuzi yasiyopendeza kwa watu wake kwa wakati fulani lakini akayashikilia kwa kujiridhisha kuwa yana maslahi na anaowaongoza. Uamuzi kama huo huwa si mwepesi. Hapo basi, kipimo kikubwa ni mapenzi ya kiongozi kwa anaowaongoza. Uadilifu unataka kiongozi awe na mapenzi, imani na huruma kwa anaowaongoza.  Uadilifu pia unamtaka kiongozi awape nafasi wananchi wake wafanye yale wayapendayo alimradi yana maslahi nao na hayaathiri maslahi ya jamii. Confucius anatufundisha tena kwenye The Analects of Confucius, 20.2:

‘Zizhang said: ‘How can one be generous without having to spend?’ The Master said: ‘If you let the people pursue what is beneficial for them, aren’t you being generous without having to spend?’

‘Zizhang alisema: ‘Vipi mtu anaweza kuwa karimu pasina kulazimika kutumia?’ Mwalimu akajibu: ‘Ukiwaachia (kuwapa uhuru) watu wafanye yale yanayowafaidisha, huwi karimu pasina kulazimika kutumia?’

Raia wakiridhika na hilo wanaweza kumwelewa kiongozi wao hata anapofanya maamuzi yanayoonekana kuwa magumu na machungu kwa wakati fulani. Nyoyo za raia zinapokuwa tulivu na roho zao zikawakinai wanaowaongoza, hapahitajiki nguvu za dola kuhakikisha utiifu wao. Kiwango hicho kikifikiwa, kiongozi huwa hatawali viwiliwili bali anatawala nyoyo za anaowaongoza.

 • Kiongozi aheshimu misingi ya uongozi wa pamoja

Uongozi ni dhamana. Maamuzi makubwa yanapofanywa kwa jina la watu yanatakiwa yazingatie maslahi yao. Serikali au chama cha siasa huchangiwa nguvu zake kwa ridhaa inayotolewa na raia au wanachama. Wao huchagua viongozi wakuu na pia huchagua wawakilishi wao katika vyombo vinavyofanya maamuzi yanayowahusu. Baadhi ya wawakilishi hao hupewa dhamana ya kusaidiana na kiongozi mkuu katika uongozi na uendeshaji wa Serikali au chama cha siasa. Katika utaratibu huo, maamuzi hufanywa kwa pamoja. Kiongozi muadilifu siyo tu anapaswa kulifahamu hilo bali pia anatakiwa aheshimu misingi ya uongozi wa pamoja. Anaweza kutofautiana na wenzake katika kufikia maamuzi, lakini alimradi mwisho wa hoja zote maamuzi yamefanywa kwa taratibu za kidemokrasia, anapaswa aheshimu maamuzi hayo na akubali misingi ya uongozi na uwajibikaji wa pamoja.

 • Kiongozi awe na busara na hekima

Maamuzi ya mtu binafsi mara nyingi humuathiri yeye binafsi au labda na watu wachache waliomzunguka. Maamuzi ya kiongozi wa kisiasa huathiri taifa zima. Changamoto za uongozi kama nilivyojaribu kuzifafanua hapa zinahitaji utulivu katika kufikia maamuzi na kuyasimamia. Jazba na hamasa mara nyingi hupelekea maamuzi ya pupa, yasiyozingatia hali halisi ya mambo na mara nyingi yenye manufaa (kama yatapatikana) ya muda mfupi tu. Kinyume chake, busara na hekima huzaa maamuzi yanayotokana na tafakuri ya kina, yanayozingatia hali halisi ya mambo na maslahi na manufaa ya muda mrefu. Kiongozi muadilifu anatakiwa ayaone haya na ayazigatie kwa kila hatua anayochukua.

 • Kiongozi awe anaijua jamii yake vilivyo

Orodha ya sifa na vigezo vya uadilifu wa uongozi imekuwa refu. Na wala sikusudii kusema mimi ni mjuzi (authority) wa fani ya uongozi wa kisiasa. Lakini uzoefu umenifundisha kuwa hata ukiyazingatia yote hayo, kama kiongozi huijui vyema jamii unayoiongoza, unaweza ukajikuta unafanya maamuzi au kuchukua hatua ambazo hazizingatii uhalisi wa mambo na hivyo kutofikia malengo yaliyokusudiwa, kama si kuirudisha nyuma dhamira nzima ya taasisi unayoiongoza. Wafuasi mara nyingi hutawaliwa na jazba na hamasa zinazotokana na uoni wao wa mambo kulingana na kiasi cha uelewa wao. Wafuasi hao wanawakilisha makundi yenye maslahi tofauti katika jamii. Kila kundi hudhani na hujionesha kuwa fikra zake ndizo zinazowakilisha jamii nzima kwa ujumla. Mara nyingi huzipandisha mno (overestimate) nguvu zao kuliko ukweli ulivyo na mara chache huzidharau na kuzidunisha (underestimate) nguvu hizo. Kiongozi mzuri ni yule anayeielewa vyema jamii yake na ambaye ameisoma na kuijua vilivyo nguvu halisi ya jamii hiyo. Kiongozi kama huyo hachukuliwi na jazba za wafuasi kiasi cha kutoona udhaifu wao lakini pia hapuuzi dhamira zao kiasi cha kutoona nguvu waliyo nayo. Akifika hapo, hatokwenda mbele wakati wafuasi hawako naye wala hatobaki nyuma wakati wafuasi wameshatangulia mbele. Kiongozi anapaswa kuwa kiongozi anayekwenda sambamba na wafuasi wake kwa kujua nguvu na udhaifu wao. Uadilifu wa uongozi hauwezi kufikiwa bila ya kulitambua hilo. Confucius kwenye The Analects of Confucius, 10.12 anasema, ‘Do not sit on a mat that is not straight,’ yaani usikae juu ya mkeka ambao haujakunjuliwa.

Kutokana na hisia mbaya zilizojengeka, imekuwa ni kawaida kuwasikia watu wakisema hakuna kitu kinachoitwa ‘uadilifu katika siasa’. Wengine husema hiyo ni hadithi ya ‘Kusaidikika’ au ndoto za Alinacha. Mimi nina mawazo tofauti. Naamini kuwa uadilifu ndiyo unapaswa kuwa msingi wa siasa, msingi wa maongozi ya kisiasa. Ikiwa siasa haiwezi kuwa na uadilifu basi itakuwa imepoteza uhalali wake wa kuwa ni njia ya kuwatumikia watu. Utumishi wa umma ni utumishi uliotukuka na unapaswa ubakie hivyo. Na msingi wake ni uadilifu.

Wanasheria wana msemo wa kusisitiza umuhimu au tuseme ulazima wa kufanya uadilifu usemao, “Let justice be done even if heaven falls” yaani “Haki na itendeke hata kama mbingu zitaanguka”. Ninavyoamini mimi ni kuwa msisitizo wa usemi huu uko katika kinyume chake yaani haki inapotendeka basi hata mbingu huzidi uimara wake. Kwa wanaoamini katika dini wanajua kuwa Uadilifu ndiyo msingi wa Ufalme wa Mbinguni. Lakini wakati kwa Mahakimu na wanasheria, msingi wa uadilifu ni katika kufuata sheria kama zilivyo, kwa maneno mengine uhalali (legality), kwa wanasiasa msingi mkuu wa uadilifu unapaswa kuwa ni kutenda haki (legitimacy) katika maamuzi hayo. Na kazi ya kuhakikisha hayo si nyepesi lakini si kitu kisichomkinika. Kama alivyosema Jaji mmoja wa Mahkama Kuu ya Uingereza akitoa maoni yake kuhusiana na hukumu ya Mahkama ya Kimataifa ya The Hague kuhusiana na shauri la ubaguzi wa rangi Afrika Kusini ambalo lilihusu zaidi mfumo wa siasa kuliko utekelezaji wa sheria pale aliposema, “It is a typical case of legality against legitimacy” yaani “Ni kesi dhahiri ya sheria dhidi ya haki”.

Kwa hivyo, kiongozi wa siasa ana dhima na dhamana ya kuhakikisha uadilifu na siyo kujificha nyuma ya pazia la sheria (kandamizi). Anaweza kufikia hapo kwa kuzingatia vigezo tulivyojaribu kuviorodhesha katika waraka huu.

 

UZOEFU WA ZANZIBAR KATIKA UADILIFU WA UONGOZI WA KISIASA

Zanzibar imepitia katika mikondo tofauti ya siasa na mikondo hiyo imezaa aina tofauti za uongozi, kila mkondo ukiahidi kubadilisha yale iliyoyaondosha. Lakini pamoja na ahadi zote hizo, kilicho dhahiri ni kwamba Wazanzibari bado hawajaonja uadilifu wa uongozi wa kisiasa. Pengine katika vipindi fulani vya historia yetu, walikaribia kufikia hapo, lakini dafrau za kisiasa ziliwarejesha nyuma na kulazimika kupiga makasia mapya kuufikia tena mlango huo.

Hakuna rekodi za kuridhisha za historia kutuwezesha kupitisha hukumu kuhusiana na hali ilivyokuwa katika tawala za kienyeji za Mwinyi Mkuu, Mwana wa Mwana au Mkama Ndume. Lakini binafsi angalau naona fakhari nilipotembelea Makumbusho ya Taifa huko Beit-el-Ajaib nilipoona tafsiri ya maneno ya Kiarabu yaliyokuwa yamenakshiwa katika ngoma ya Mwinyi Mkuu ambayo ilikuwa mojawapo ya alama ya utawala (symbol of power) ikisema “Mtawala mwema ni yule anayewatendea mema watu wake, akawaridhisha, ikiwa ni pamoja na wale wanaotofautiana naye kifikra.” Huu ndiyo unaoitwa ‘utawala bora’ katika zama hizi. Wazanzibari walishayakubali karne kadhaa zilizopita. Huu ndiyo ustaarabu. Suala linakuja, Je, huu ni ushahidi wa kuwepo uadilifu wa uongozi wa kisiasa zama hizo? Au ni kauli za dhamira tu ambazo hazikuzingatiwa katika uendeshaji wa nchi?

Kipindi kilichofuata kilikuwa cha kuja kwa tawala za kigeni, kwanza Wareno, halafu Waomani na baadaye Waingereza. Tawala hizi zilikuwa na vitimbi vyake lakini hazikuacha athari mbaya mara zote labda ukiondoa Wareno ambao ukhabithi wao unafahamika vyema kote katika mwambao wa Afrika Mashariki. Miongoni mwa Masultani wenye asili ya Kiomani (natumia neno hili kwa makusudi kwani watawala hawa baadaye walizaliana na wenyeji na kuwa sehemu ya Waswahili) walikuwemo watawala waliokuwa na kiburi kama Sayyid Hamoud bin Mohammed (1897 – 1902) ambaye ziko hadithi nyingi za mapokeo zinazoonesha udhalilishaji wa raia wake mmoja mmoja (wakiwemo hata Waarabu) lakini walikuwemo pia watawala wema kama Sayyid Khalifa bin Haroub (1911 – 1960) ambaye anasifika kwa kuongoza nchi kwa uadilifu mkubwa kiasi cha kukubaliwa na wote, ASP na ZNP, pale siasa za vyama zilipoingia Visiwani katika miaka ya ’50.

Hata wakoloni wa Kiingereza nao walilaumiwa kwa kuwagawa wananchi kwa misingi ya kikabila na kupandikiza mbegu za chuki ambazo zinaendelea kuiathiri Zanzibar hadi sasa lakini pia wanakumbukwa kwa kuweka misingi ya Mahkama huru zilizozingatia usawa wa watu wote mbele ya sheria.

Ukoloni ulifuatiwa na harakati za kudai uhuru ambao uliahidi kuwakomboa Wazanzibari na kuleta uongozi mwema kwa kuja na Katiba nzuri yenye kuingiza kikamilifu Tamko la Haki za Binadamu (Bill of Rights) lakini hatua za awali katika Serikali ya madaraka ya ndani (internal self-government) zilionesha dalili mbaya. Mnamo mwezi Agosti 1963, Serikali ya ZNP/ZPPP ilipitisha sheria mbili za kikandamizaji, zote zikimpa madaraka makubwa Waziri wa Mambo ya Ndani, moja kupiga marufuku chama au jumuiya yoyote na nyengine kufuta magazeti ikiwa tu ‘ataona vinakwenda kinyume na misingi ya uongozi mwema katika nchi’. Maamuzi ya ipi ni ‘misingi ya uongozi mwema’ ilikuwa ni ya Waziri bila ya kufungwa na masharti mengine yoyote.

Uhuru wa Desemba 10, 1963 ukafuatiwa na Mapinduzi ya Januari 12, 1964 ambayo yalifanywa kwa jina la kuwakomboa Wazanzibari na ‘kuleta usawa na kufuta aina zote za ubaguzi na ukandamizaji katika nchi’. Rekodi ya Serikali za Awamu ya Kwanza ya Mapinduzi chini ya Rais Abeid Amani Karume (1964 – 1972) hazioneshi kufikiwa kwa malengo hayo. Yalikuwepo mafanikio yaliyolenga kufikiwa kuleta umoja na usawa kwa kunyanyua hali za maisha ya watu wa chini katika nchi lakini kutokana na nguvu kubwa iliyotumika kuyafanikisha, mafanikio hayo yalifunikwa na madhila makubwa yaliyopitishwa kwa raia. Watu wasio na hatia waliuawa, waliwekwa vizuizini na kuteswa kwa kudhaniwa tu kuwa wanaipinga Serikali, Mahkama huru zilifutwa, uhuru wa vyombo vya habari ulitiwa kitanzi, na watu wakaachiwa waishi katika dhiki kubwa za kiuchumi na kijamii (Marehemu Ali Nabwa aliwahi kuandika kuwa Zanzibar ilikuwa nchi ya foleni).

Siku za mwanzoni za Awamu ya Pili chini ya Sheikh Aboud Jumbe (1972 – 1984), hali ilianza kutengamaa kwa kuanzisha Katiba na Baraza la Wawakilishi lakini baadaye makundi yalianza na vitendo vya ukandamizaji vikaanza kujirejea. Utulivu wa muda mfupi uliokuja na Awamu ya Tatu (1984 – 1985) ambapo Wazanzibari walianza kuamini kuwa wameanza kufika walikokusudia uliingia katika majaribu makubwa pale Sheikh Ali Hassan Mwinyi alipochaguliwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na mahala pake kuchukuliwa na Marehemu Sheikh Idris Abdulwakil, kiongozi aliyekuwa na uadilifu wa nafsi lakini udhaifu wake kiuongozi katika Awamu ya Nne (1985 – 1990) ukatumiwa kumyumbisha na kufanikisha malengo ya waliojisogeza karibu naye.

Matumaini mapya yalijengwa kwa uongozi wa Awamu ya Tano chini ya Rais kijana wakati huo, Dk. Salmin Amour (1990 – 2000), lakini jazba na hamasa ya kulipiza visasi kwa wale walioonekana wana mawazo tofauti kisiasa na yale ya Serikali yake vilipelekea mafanikio yaliyoanza kupatikana kiuchumi kuvurugika kutokana na migogoro ya kisiasa.

Kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992 kulipokewa kwa hisia tofauti na raia. Wale waliokuwa wakitaka mabadiliko walikuwa na matumaini makubwa na wale waliokhofia mabadiliko walikuwa katika tahadhari kubwa. Wanasiasa wakatumia udhaifu na uelewa mdogo wa wanaowaongoza kuwapotosha ili kufikilia matakwa yao binafsi na Zanzibar ikashuhudia kipindi kibaya cha ukiukwaji wa hali ya juu wa haki za binadamu na kupondwa pondwa kwa misingi ya uadilifu wa uongozi.

Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Amani Abeid Karume (2000 hadi sasa) ilitarajiwa ingeweza kuja na mwanzo mpya na kupoza majeraha ya kihistoria iliyoyarithi lakini bahati mbaya hilo lilishindikana katika miaka ya awali ya utawala huo.

Hali ilibadilika ghafla kuanzia Novemba 5, 2009 pale Rais wa Zanzibar, Mhe. Dk. Amani Abeid Karume na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, walipofanya mazungumzo katika Ikulu ya Zanzibar na kuzaa kile kinachojulikana sasa kama ‘Maridhiano’.  Rais Amani Karume amejihakikishia nafasi yake katika historia ya Zanzibar kwa kuchukua hatua ya kijasiri ya kuwapatanisha na kuwaunganisha. Wazanzibari sasa wamejenga matumaini mapya na makubwa kutokana na Maridhiano hayo huku wakitaraji kufuli za lango la chuma linalozuia uadilifu wa kisiasa kuingia ndani ya visiwa zitavunjwa daima na Zanzibar itashuhudia historia mpya ikiandikwa.

Unapozingatiwa mtiririko huo wa matukio na mwenendo wa viongozi wetu mtu ataona kuwa vigezo vyote vya kiongozi muadilifu vikiwemo vile kwamba kiongozi anatakiwa azingatie maslahi ya nchi na watu wake hata kama watu wataona anayoyafanya hayana maslahi nao kutokana na ufinyu wa taarifa, anatakiwa awe mfano kwa anaowaongoza, anatakiwa atembee juu ya maneno yake, azingatie umoja, amani na utulivu katika nchi, azingatie haki na uadilifu kwa anaowaongoza (wanaomkubali na wasiomkubali) na asikubali kuona ukandamizaji wa aina yoyote, awapende anaowaongoza, aheshimu misingi ya uongozi wa pamoja, awe muumini wa kweli wa demokrasia, na awe na busara na hekima, kwa muda mrefu vililikuwa vimepuuzwa. Lakini sasa hali imeanza kubadilika na upepo wa kheri umeanza kuvuma kuelekea visiwa vya Zanzibar ukibeba hewa safi inayopulizia uhai mpya kwa nchi ya Zanzibar.

Lakini kwa nini ilikuwa hivyo kwa muda mrefu? Kwa nini matumaini ya Wazanzibari yalikuwa yakipotezwa kila mara yalipojengwa? Kwa nini watawala wetu walishindwa kuwapatia Wazanzibari uongozi unaozingatia uadilifu pamoja na kuahidi hivyo kila mabadiliko yalipotokea. Jawabu pengine analo Sheikh Abdilahi Nassir wa Kenya pale alipozungumzia mwenendo wa watawala wa Afrika katika waraka wake ‘Liberation Theology: The Islamic Perspectives’:

“We only need to cast a cursory glance at our leaders’ lives, after taking over the reins of government, for us to realise that what was concealed in their hearts – consciously or unconsciously – at the time of the struggle for independence, was not what the masses had in mind; otherwise how do we rationalise the misuse of the millions of foreign exchange, earned from the sweat of the common people in importing military equipment and ammunition – not in defence of the motherland against foreign aggression, but in entrenching themselves in their positions and killing those who would dare question them or protest against their abuses of power? How do we rationalise the importation of the many luxuries that the common people cannot, and will never enjoy during their lifetime, while hospitals are without medicine, schools without books and desks, and while families do not know when to expect their next meal? Indeed is it not true that most of our rulers today earn far bigger salaries, and enjoy many more facilities, than their colonial predecessors – even taking the inflation factor into account? Is not all this at the expense of the common man?

But once again, why should this be so?

Well, in the words of the Qur’an (28:79), it is because they wished they had “the like of what Qarun has got”! …

By admiring Qarun, some of his people assumed his arrogance. Equally, by wanting to be like our colonial masters, most of our leaders have developed their values and tastes, and assumed their pomp. In some cases they have allied themselves with the ex-colonialists in plundering our continent under the guise of ‘partnership in development’. However, by not having the confidence the colonial masters had, they have become so sensitive to the slightest challenge to their authority. Hence, the abuse of power we see almost all over our continent in the form of the violation of human rights.”

 

MATOKEO YA KUPUUZWA MISINGI YA UONGOZI WA UADILIFU KATIKA SIASA

Dunia kwa ujumla hivi sasa inashuhudia mmong’onyoko wa imani kwa wanasiasa. Wananchi wanahisi wamedanganywa sana na kusalitiwa kiasi cha kuona kuwa wanasiasa wote ni sawa sawa, jora moja mkasi mmoja. Hawaamini kama kutakuwa na tofauti hata kama watabadilisha uongozi kwani kila waliyemuanini amewaangusha. Imani kwa viongozi ikiondoka basi na ule msingi wa amana (trust) ambao, kama tulivyoona, ndiyo msingi mkuu wa maongozi ya nchi nao hundoka. Hali hiyo ya kupoteza matumaini ni hatari kwa sababu bado hakuna mbadala wa siasa kama njia ya kuufikia uongozi wa nchi.

Mfano mzuri sana wa karibuni wa jinsi maamuzi yasiyozingatia misingi ya uadilifu yanavyoathiri mitazamo ya raia kwa viongozi wao unapatikana kwa Waziri Mkuu wa zamani Uingereza, Tony Blair. Likifanya tathmini ya mtazamo wa raia kwa kiongozi huyo ambaye nilibahatika nikiwa Uingereza mwaka 1997 kushuhudia jinsi alivyopendwa na kuaminiwa na Waingereza, jarida linaloheshimika la The Economist la Mei 1218 2007, linaandika:

“Few Britons, it seems will shed a tear when Tony Blair leaves the stage on June 27th after a decade as prime minister, as he finally said this week he would. Opinion polls have long suggested that he is unpopular. On May 3rd local and regional elections gave voters a last chance to give Mr Blair a good kicking. They took it with both feet, handing power to Conservatives, Scottish Nationalists, Welsh nationalists, anybody but distrusted Labour. Most wish he had gone last year – an opinion shared by his likely heir, Gordon Brown, who now faces a mighty struggle against David Cameron’s Tories.

Either Britons are an ungrateful lot, or Mr Blair deserves his shabby send-off for having delivered too little and disappointed too much. The truth, as usual, is more complicated.

… [Mr Blair], after all, was the most gifted politician of his generation – certainly in Europe and (depending on your opinion  of the foxier but less disciplined Bill Clinton) perhaps wider than that. Before coming to power Mr Blair already had one enormous achievement to his name: dragging the Labour Party to the electable centre. In 1997 he had not just a big parliamentary majority but a country that wanted what he wanted – an economy that combined the hard-won gains of Thatcherism with a greater emphasis on social justice and modernised public services. How could he fail?”

 

Tony Blair ‘alilewa’ na imani aliyopewa na Waingereza, akajiamini kupita kiasi kwamba angeweza kufanya lolote na bado akaendelea kupendwa, akadhani anaweza kwenda mbele na kuuwacha umma nyuma, akashindwa kufanya mahesabu ya maslahi bora kwa Uingereza kwa wakati fulani, akaitia nchi vitani kwa taarifa zisizo sahihi na zilizopotoshwa kwa makusudi. Matokeo yake ni machungu siyo kwa Uingereza tu bali kwa ulimwengu mzima. Hiyo ndiyo athari ya kutozingatia uadilifu katika uongozi wa kisiasa.

Hapa kwetu Zanzibar, mfano mzuri wa mwanasiasa aliyepoteza fursa adhimu kama hii nadhani ni Dk. Salmin Amour. Aliingia madarakani wakati Zanzibar imo katika mgawanyiko mkubwa wa kisiasa kufuatia Maalim Seif Sharif Hamad kuondolewa katika nafasi ya Waziri Kiongozi na baadaye kufukuzwa kutoka CCM na kuwekwa ndani kwa mashtaka ya kubambikiziwa. Watu wakampa nafasi ya kurejesha umoja na matumaini katika nchi. Alianza vizuri katika uwanja wa uchumi na kipindi chake kikashuhudia Maalim Seif kupewa dhamana na kutolewa kutoka gerezani, akaanzisha mawasiliano ya kimya kimya na Maalim Seif ambayo yalikusudiwa yalete siasa za maelewano. Ghafla akageuka. Mawasiliano yakakatika, akaanza mashambulizi makali na vitisho dhidi ya mwenzake na baadaye dhidi ya wapinzani wote, Zanzibar ikashuhudia utawala wa mkono wa chuma, na baada ya uchaguzi  mkuu wa 1995, mgogoro mkubwa wa kisiasa. Hatimaye juhudi za Chief Emeka Anyaoku wa Jumuiya ya Madola zikaleta Muafaka mwaka 1999. Dk. Salmin akapata fursa ya pekee mwaka mmoja tu kabla ya kumaliza muda wake wa Urais kuwapa Wazanzibari zawadi ya umoja, amani na utulivu. Akatoa hotuba safi katika viwanja vya Ikulu, Juni 9, 1999 ambayo ikiambatana na kitendo chake cha kukumbatiana na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif, iliibadilisha Zanzibar na kubadilisha mahusiano ya wafuasi wa CCM na CUF ndani ya usiku mmoja tu. Akasema:

“Lakini lazima tuseme wazi kabisa, tuelewane ili Muafaka huu uote mizizi na usonge mbele. Siwezi kuwa shahidi wa Muafaka ambao umehusisha watu wakubwa kama huyu mwenzetu Ndugu Anyaoku, kwa miaka minne, halafu baada ya siku tatu ukaelea na maji. Itakuwa haina maana yoyote. Dhamana itakuwa mimi na Maalim Seif, ama yeye au mimi. … Na mimi natamka nitautekeleza na kuusimamia Muafaka huu na maelewano haya kwa uwezo wangu wote, kwa sababu hapa hapana suala la ushindi kwamba fulani kashinda, fulani kashindwa. Hapa tunazungumzia nchi kwa hivyo sote tumeshinda.”

Hakuishia hapo bali aliendelea kusisitiza:

“Natumai kwamba kuanzia sasa, watu wa Tumbatu, watu wa Shangani, watu wa Malindi, watu wa Makunduchi, wa Kisiwa Panza, wa Mkoani, wa Mtambwe, wa Kidombo, wa kila mahali mtakuwa kitu kimoja kufanya kazi ya uzalendo wa taifa letu, maana uzalendo ni nchi. Chama ni ushabiki. Chama hupita, nchi haiondoki, kwa hivyo ukiamua kwamba usahau nchi ushikilie chama tu, ukagombana na watu, ukaleta uhasama, ukaleta chuki, chama kuna siku kitakuwa hakipo, nchi haiondoki, kwa hivyo lazima tutafautishe baina ya uzalendo na ushabiki. Kwa hivyo wakereketwa wale ambao jazba zimewakaa kila wakati watambue wakati wa ushabiki wa siasa sawa, ukifika uzalendo sote tuwe kitu kimoja, alie Dar es Salaam, tuwe kitu kimoja, alie Tanga kitu kimoja, alie Mombasa kitu kimoja, alie Dubai kitu kimoja, alie Denmark, alie Sweden, alie London sote kitu kimoja. Huu ndio uzalendo.”

Matumaini haya yalipotezwa na nchi ikarudi katika mgogoro mkubwa zaidi pale Dk. Salmin Amour alipoyageuka maneno yake mwenyewe katika mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Kibanda Maiti, Zanzibar wiki moja tu baadaye. Majeraha ya kisiasa tuliyokuwa nayo kabla ya kufikiwa kwa Maridhiano ya Wazanzibari Novemba 5, mwaka jana yalitokana na kitendo hicho cha Dk. Salmin kuigeuka dhamira yake. Confucius anasema ‘A gentleman would be ashamed should his deeds not match his words’ yaani muungwana anapaswa kuona aibu iwapo vitendo vyake havilingani na kauli zake.

 

HITIMISHO

Uongozi wa kisiasa si jukumu dogo ingawa siku hizi unaonekana ndiyo kimbilio la kila aliyefeli maisha katika nchi yetu. Si ajabu basi ikawa dhima na dhamana za uongozi wa kisiasa zimekuwa haziheshimiwi na uadilifu umepotea. Lakini kama tulivyotangulia kusema, uongozi wa nchi unatokana na amana ambayo hutolewa na wananchi. Hivyo, badala ya wananchi kukata tamaa na viongozi wao, wanapaswa kubeba jukumu lao la kudai uadilifu huo ikiwa ni marejesho ya amana waliyotoa. Hiyo ni changamoto kwa wananchi.

Kwa upande mwengine, viongozi wa kisiasa nao wanapaswa wachukue hatua kujisafisha na kusafisha nyumba zao ili kurejesha imani ya wananchi kwao na kwa uongozi wao. Msingi wa kufanya hivyo ni kujichunguza na kujisahihisha. Huo ndiyo unapaswa kuwa msingi hasa wa utawala wa kidemokrasia tunaoupigia chapuo kwamba tunaufuata. Fareed Zakaria, mchambuzi wa masuala ya siasa anayeheshimika ulimwenguni, katika kitabu chake ‘The Future of Freedom: Illiberal Democracy at Home and Abroad’,  Uk.256 anasema:

“Modern democracies will face difficult new challenges … and they will have to make their system work much better than it currently does. That means making democratic decision-making effective, reintegrating constitutional liberalism into the practice of democracy, rebuilding broken political institutions and civic associations. Perhaps most difficult of all, it requires that those with immense power in our societies embrace their responsibilities, lead, and set standards that are not only legal, but moral. Without this inner stuffing, democracy will become an empty shell, not simply inadequate but potentially dangerous, bringing with it the erosion of liberty, the manipulation of freedom, and the decay of a common life.”

Turudi katika mstari kwa kuzingatia ipasavyo misingi ya uadilifu wa uongozi. 

Kuyafanikisha hayo, panahitajika mafahamiano mapya ya mahusiano kati ya waongozi na wangozwa. Haya yanaweza kupatikana kwa kuwa na Dira ya Taifa itakayowaunganisha wote (Common Vision for All).

Ni mapendekezo yangu kuwa dira hiyo ipatikane kwa kuandikwa Katiba mpya ya Zanzibar kupitia utaratibu utakaowashirikisha wananchi wote. Katiba hiyo mpya itafsiri upya misingi ya amana (trust) ambayo wananchi wanaipa mihimili mitatu ya Dola inayosimamia maongozi ya nchi – Mamlaka ya Utendaji (Serikali), Mamlaka ya Kutunga Sheria (Baraza la Wawakilishi) na Mamlaka ya Utoaji Haki (Mahkama). Wakishirikiana waongozi na waongowa, hakuna lisilowezekana. Cha kuzingatia ni wote kukubali kwamba “Politics is the art of the possible” (Siasa ni sanaa ya yanayomkinika) na “Politics is an art of compromise” (Siasa ni sanaa ya suluhu).

Tukubali tu kuwa njia ya kusonga mbele ni kukubali kutofautiana katika fikra lakini tubaki kuwa wamoja. Uzalendo wa nchi utuunganishe. Tufahamu siasa si lengo, ni njia tu ya kufikia lengo. Lengo ni utumishi wa umma kwa kuyatimiza matarajio yao. Malengo ya utumishi huo wa umma ambayo ndiyo malengo ya Serikali yoyote inayothamini raia wake yanapaswa nayo kufafanuliwa na kuwa mwongozo wa Taifa. Yaliwekwa vizuri sana na Mzee Abeid Amani Karume katika Manifesto ya ASP ya 1961 katika kueleza tafsiri ya Uhuru unaopiganiwa:

“UHURU ndio msingi wa siasa ya chama chetu. Unachanganya bila ya shaka kumalizika kwa Serikali ya Kikoloni na mwisho wa utawala wa nje. Kadhalika UHURU unakusanya ukunjufu kutokana na ujinga na haja zisizokwisha. UHURU wa kuwa na pato la kumwezesha mtu kuyatekeleza yaliyombidi, kustarehe na kuwa mtu, UHURU wa kuishi kama watu katika nchi yetu.

Huu ndio UHURU ambao daima tukiutaka, huu ndio UHURU ambao daima twaupigania, huu ndio UHURU ambao tumejitolea kuutumikia na siku zote tutautumikia kwa nguvu zetu zote na kwa uwezo wetu wote.

Tunadhani kuwa kila mmoja wetu katika visiwa hivi aendelee mbele kwa mujibu wa uwezo wake, jambo ambalo ni gumu lakini kabisa si jambo lisilowezekana. Na iwapo wewe kililahi huyapingi haya tuliyoadhimia na wewe mwenyewe ndiye uwezaye kujua, basi tafadhali karibu uungane nasi twende pamoja na kuutia mkononi huu UHURU.”

Wazanzibari tunapaswa kujiuliza siasa tuliyo nayo kwa kiasi gani imetufikisha katika malengo hayo aliyoyaeleza Mzee Karume? Ni wangapi kati yetu tunaishi tukiwa na ukunjufu kutokana na ujinga na haja zisizokwisha? Ni wangapi tunamiliki pato la kumwezesha mtu kuyatekeleza yaliyombidi, kustarehe na kuwa mtu, kuishi kama watu katika nchi yetu? Ni wangapi kati yetu katika visiwa hivi tuna nafasi ya kuendelea mbele kwa mujibu wa uwezo wetu badala ya kutegemea ukoo gani tunaotoka? Je, tumefikia kiwango cha UHURU ambao daima tukiutaka, daima tukiupigania, na ambao tulijitolea kuutumikia na kuahidi kuwa siku zote tutautumikia kwa nguvu zetu zote na kwa uwezo wetu wote? Jawabu analo kila mmoja wetu.

Uongozi ni utumishi wa umma. Umma lazima usimame kwa njia za amani kabisa kudai uadilifu wa uongozi kutoka kwa wanaowaongoza. Viongozi wakiona wananchi wamechachamaa watabadilika. Wasipobadilika watapeperushwa na upepo wa mabadiliko. Tukifikia hapo, heshima ya siasa kama fikra, busara na mipango ya kuendesha nchi itarudi.

 

REJEA:

Joseph Mihangwa, ‘Kuuawa kwa Rais Abeid Amani Karume: Ni Mapinduzi au Chuki Binafsi?’, Rai (Dar es Salaam), Mei 2430, 2007.

Marcus Tullius Cicero, The Republic, kama ilivyonukuliwa katika Chris Paten (1998), East and West, Macmillan (London).

John Uhr (2003), ‘Creating a Culture of Integrity’, The Second Publication in the series “Taking Democracy Seriously”, Commonwealth Secretariat (London).

Kieron O’Hara (2004), Trust: From Socrates to Spin (Icon Books: Cambridge).

Jean-Jacques Rousseau (1993), The Social Contract and Discourses (trans. G.D.H. Cole, rev. J.H. Brumfitt and John C. Hall, upd. P.D. Jimack) (Everyman: London)

Brian Skyrms (1996) Evolution of the Social Contract (Cambridge University Press: Cambridge).

Rudolph Giuliani (2002), Leadership (Little, Brown, London).

Abdilahi Nassir (1991), ‘Liberation Theology: The Islamic Perspectives’ , Waraka uliowasilishwa katika Mkutano wa Kimataifa wa kujadili Ukombozi wa Pili wa Bara la Afrika, uliofanyika Februari 1991 mjini London.

‘How will history judge him?’, The Economist (London), May 12th18th 2007.

Salmin Amour (1999), Hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Salmin Amour kwenye Karamu Rasmi ya kutiwa saini Makubaliano baina ya CCM na CUF, Ikulu – Zanzibar tarehe 9.6.99, (Government Printers, Zanzibar).

Fareed Zakaria (2003), The Future of Freedom: Illiberal Democracy at Home and Abroad (W.W. Norton & Company, New York, London).

Abeid Amani Karume (1961), Manifesto ya ASP, (Zanzibar).

The Analects of Confucius.


* Msaidizi Maalum wa Katibu Mkuu wa CUF katika Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kimataifa, Waraka uliowasilishwa katika Semina ya Katiba, Sheria na Maendeleo ya Zanzibar iliyoandaliwa na Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar kwa ajili ya Vyama vya Siasa, tarehe 30-31 Mei, 2007 katika Ukumbi wa Ofisi ya Umoja wa Watu wenye Ulemavu, Wireless, Zanzibar. Waraka huu umefanyiwa marekebisho machache kuingiza matukio ya hivi karibuni katika siasa za Zanzibar hasa suala la Maridhiano.