ismailjussa

Mizengwe ilinitoa Chadema – Mwera

In Uncategorized on September 7, 2010 at 9:44 pm

Aliyekuwa Mbunge wa Tarime, Charles Mwera, akipokelewa na Naibu Katibu Mkuu wa CUF ambaye pia ni Mgombea mwenza wa Urais wa Jamhuri ya Muungano, Juma Duni Haji, siku yeye na viongozi wenzake Chadema wa Wilaya ya Tarime walipotangaza kukihama chama chao na kujiunga na CUF. (Picha kwa hisani ya http://www.wavuti.com)

Tuesday, 07 September 2010 17:09

Na Salim Said

KAMBI ya wabunge walioangushwa katika kura za maoni katika vyama vyao na kuamua kutimkia vyama vingine vya siasa na kuwania ubunge imezidi kuwa kubwa.

 Hivi karibuni  aliyekuwa mbunge wa Tarime (Chadema), Charles Mwera alijiunga na wanachama wengine waliotimka katika vyama vyao  baada ya  kuhamia Chama cha Wananchi (CUF) na kuweka bayana kwamba mizengwe na ufisadi ndani ya chama hicho  ndio  sababu ya yeye kutimkia CUF.

Anasema mizengwe na ufisadi huo ulitokea  wakati wa mchakato wa kuteua wagombea wa ubunge na udiwani watakaopeperusha bendera ya Chadema katika uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 31 mwaka  huu.

Mwera alikabidhiwa  kadi ya uanachama wa CUF na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Zanzibar ambaye pia ni mgombea mwenza, Juma Duni Haji, katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya Chama hicho Buguruni Agosti 15 mwaka huu.

“Nakukabidhi kadi hii, ili tushirikiane pamoja katika kutetea haki za wanyonge na kuleta mabadiliko ya kweli Tanzania na kwa kuwa kadi hii nimeisaini mimi basi saini yangu itabakia milele Tarime,” anasema Duni.

Akieleza kilichomkimbiza   Chadema, Mwera anaweka bayana kuwa, amehama chama hicho kutokana na mizengwe iliyoongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho,  Freeman Mbowe.

Anasema Chadema kinajinadi kwa kupambana na ufisadi na kutetea haki, lakini ndani yake kina mizengwe na ufisadi mkubwa unaofanywa   na viongozi wa chama hicho  kuwaweka baadhi ya watu madarakani.

“Chadema kinajidai kupiga vita ufisadi lakini kimejaa mizengwe.  rushwa na hongo zilitumika kuhakikisha mimi  sirudi  kupeperusha bendera ya chama, kwa kweli sikuridhika hata kidogo,” anasema Mwera.

“Hata nilipokata rufaa, Mbowe alilazimisha rufaa iamuliwe kwa kutumia kura za wazi. Katiba ya Chadema inampa mwenyekiti nafasi ya kuteua wajumbe sita wa kamati kuu, hivi mtu anajua umemteua atapiga kura ya huru kupinga kura ya wazi,” anahoji Mwera.

Aliongeza, “Haiwezekani mtu anatuhumiwa kwa rushwa na kuhonga wanachama vitu mbalimbali ili achaguliwe, halafu anahukumiwa kwa kutumia kura ya wazi ndani ya kamati kuu. Hii ni mizwenge iliyotumika kuning’oa.”

Mwera aliangushwa katika kura za maoni za kugombea ubunge wa Tarime na Mwita Waitara, ambaye amepitishwa kupeperusha bendera ya chama hicho jimbo la Tarime.

“Mbowe alikuwa na mgombea wake na alisema kwamba hata kama Tarime itaenda kwa vyama vingine  lazima mtu wake apite. Kimsingi haki haikutendeka katika mchakato wa kutafuta wagombea Tarime,” anasema Mwera.

Anasema baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu akiwamo Profesa Mwesiga Baregu walipendekeza Mwera apewe bendera ya Chadema Tarime lakini  Mbowe  hakuwa tayari.

Mwera anasema wananchi wa Tarime  na wanachama wa  CUF wanatakiwa kutambua kuwa  jimbo hilo halitarudi CCM bali litaendelea kubakia katika kambi ya upinzani ili kuendeleza yale aliyoyaanzisha kabla na baada ya mbunge.

“Nitaipeperusha bendera ya CUF na kuhakikisha kwamba jimbo tunalichukua. Najua nimetoka kwa wapambanaji na nimeenda kwa wapambanaji wengine kuendeleza mapambano. Jimbo la Tarime tulilipata kwa mapambano na CUF,” anasema Mwera.

Anasema  ana uhakika wa kuibuka na ushindi kwa kuwa ni mwanasiasa anayejali matatizo ya wananchi jambo ambalo lilisababisha ashinde  katika uchaguzi mdogo uliofanyika baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema, Chacha Zakayo Wangwe.

“Unajua chama ni njia tu lakini wanaomweka mgombea  madarakani si wanachama wa chama husika ni wananchi ambao bado wananihitaji ndio mana nikachagua njia ya kuja CUF,” anasema  Mwera.

Anasisitiza kuwa, ameamua pia kuhama Chadema kwa sababu inafanya makosa yanayofanywa na CCM kwa kuweka wagombea wasiokubalika na kuendeleza uchafu wa ufisadi.

“Mimi ni mtu wa dini, nina msimamo, hata humu ndani ya CUF  hata siku moja sitatumia fedha kutafuta madaraka,” anasema Mwera.

Mwera anasema anajivunia mabadiliko makubwa aliyoyaleta katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, ikiwa ni pamoja na kufuta hati chafu, kupata sh7 bilioni kama ruzuku ya serikali kuu kwa ajili ya maendeleo na kufanikisha wazee kuweza kuwalipia ada ya shule watoto wao.

Mkurugenzi wa Mipango wa CUF, Shaweji Mketo anasema wamemfungulia Mwera milango ya kugombea ubunge wa Tarime kwa kuwa kanuni zao zinaruhusu.

“Huyo aliyeteuliwa na chama kugombea ubunge wa Tarime ndio alikuwa akipiga simu kila siku akitaka nafasi hiyo apewe Mwera na alikubali kabisa kuwa Meneja wake wa Kampeni wa Mwera,” anasema Mketo.

Akizungumzia kitendo cha Mwera kuhamia CUF, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe anasema Mwera alitaka huruma ya Wajumbe wa Kamati Kuu bila ya kuwa na sababu za msingi za kuishawishi, baada ya kuangushwa na wanachama katika kura ya maoni.

 “Sitaki malumbano yoyote na Mwera ambaye si mwana-Chadema tena. Hana njia yoyote ya kunilaumu nadhani  anafahamu mchakato wa kupata wagombea ndani ya chama, kama anakubalika na wananchi wa Tarime kwa nini hawakumchagua,” anahoji Mbowe.

Kuhusu tuhuma ya kuendesha kura ya wazi, Mbowe anasema ndani ya Kamati Kuu ya Chadema mtindo huo ni wa kawaida na hawana cha kuficha.

“Mwera alikataliwa na wanachama sio mimi, alikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri na baadaye mbunge. Tunamtakia safari njema CUF,” anasema Mbowe.

Source: Mwananchi

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: