ismailjussa

Serikali ya CCM imeshindwa kutimiza ahadi

In Michango Bungeni on July 11, 2010 at 3:28 pm

 

 

MCHANGO WANGU BUNGENI WAKATI WA KUJADILI HOTUBA YA BAJETI YA OFISI YA WAZIRI MKUU TAREHE 16 JUNI, 2010

 

Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana. Tunajadili hotuba ya Bajeti ya Waziri Mkuu ambaye kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 52, Ofisi ya Waziri Mkuu, ndiye mwenye dhamana ya kusimamia, udhibiti, usimamiaji na utekelezaji wa shughuli za siku hadi siku za Serikali ya Jamhuri ya Muungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo tunapozungumzia Ofisi ya Waziri Mkuu tunazungumzia kwa hakika utendaji wa Serikali nzima iliyopo hapa na kwa sababu hotuba ya Waziri Mkuu ilijikita katika kufafanua mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Nne yakielezwa kwamba ni utekelezaji wa Ilani ya CCM, ningeomba na mimi nijikite hapo kuitathmini Serikali hii kwa miaka minne imefanya nini katika kutekeleza ahadi zake na kama kweli inastahiki sifa ambazo zimeelezwa hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa mkononi ninayo Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ambayo imekuwa gumzo kubwa humu ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 157 kifungu cha 126 inasema, na naomba kunukuu: “Ilani hii ya CCM ya mwaka 2005–2010 inatangaza vita ya kuutokomeza umaskini nchini Tanzania. Utekelezaji wa dhati wa majukumu makuu mawili yaliyoainishwa na Ilani, yaani kujenga msingi wa uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea na kuwawezesha wananchi kiuchumi ndiyo njia ya uhakika ya kuutokomeza umaskini hatua kwa hatua. Tangazo hili la vita dhidi ya umaskini ni ahadi iliyotolewa na CCM kwa wananchi kwamba wakiichagua tena itaongoza mapambano hayo dhidi ya umaskini katika nchi yetu.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nasikitika sana kusema kwamba ukitazama hali halisi malengo hayo ya Ilani yameshindwa, na nitathibitisha maneno yangu, naomba wenye jazba kidogo wazitulize. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ukurasa wa 159 wa Ilani hiyo, kwa sababu Ilani hii nimeisoma sana mimi na haikunivutia ndiyo maana nikaamua kubakia CUF mpaka leo, inasema kwamba utekelezaji wa haya unapaswa kuwa wa vitendo. Mheshimiwa Mbunge mmoja hapa amesema kwamba Serikali hii imefanya maajabu. Mimi nataka nikubaliane naye kabisa kwamba imefanya maajabu kabisa katika kuzidi kuporomosha maisha ya Watanzania! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma hapa inazungumzwa kwamba malengo mawili makubwa ni kujenga uchumi wa kisasa na kuondokana na utegemezi, lakini tunapotazama hali halisi, tunaona kwamba utegemezi haujaoondoka na ushahidi wa wazi ni bajeti hii ya mwaka huu ambayo imepitishwa hapa juzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii vyanzo vya ndani ni trilioni 6 tu kati ya trilioni 11 ambazo zinategemewa zitumike, maana yake ni kwamba kiasi kikubwa zaidi kinategemea kutoka katika ufadhili au kuendelea kukopa. Hii maana yake ni kwamba suala la utegemezi bado liko pale pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini zaidi katika suala la ujenzi wa uchumi, inasikitisha kwamba miaka mitano hii hata yale mafanikio machache yaliyokuwa yamefikiwa hadi kufikia mwaka 2005 chini ya Serikali ya Awamu ya Tatu nayo pia yamepotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano Awamu ya Tatu ilipochukua Serikali ilikuta uchumi unakua kwa asilimia 3.6 lakini wakati inaondoka madarakani ikauacha uchumi unakua kwa asilimia 6.7. Lakini leo kwa takwimu hizi tunaambiwa uchumi unakua kwa asilimia 6.9 maana yake mafanikio kwa miaka mitano yote ni kuongeza asilimia 0.2 na tena ukuaji wenyewe unaonekana ni wa vitabuni zaidi kuliko uhalisia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini zaidi unauona utendaji wa Serikali hii tunapoangalia suala la mfumuko wa bei, ambao ndiyo unamuathiri mwananchi sana, kwa sababu unazungumzia kuongezeka kwa bei ya bidhaa ambazo anazitumia kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Serikali hii inaingia madarakani ilikuta Serikali ya Awamu ya Tatu imefanikiwa kushusha kiwango cha mfumuko wa bei kutoka 27% mwaka 1995 hadi 4.5% lakini juzi Waziri mwenyewe ametwambia hapa kwamba sasa mfumuko wa bei mwaka uliopita umerudi kuwa 12.2%. Haidhuru wametuambia kwamba kuna takwimu zinazoonesha kwamba eti mfumuko wa bei unaendelea kushuka lakini tunapozitazama bei za vitu halisi huko mtaani hazioneshi hali hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuthibitisha hoja yangu zaidi tunapoangalia Uchunguzi wa Bajeti ya Kaya (Household Budget Survey) wa mwaka 2007, unasema mfumuko wa bei ukitazamwa katika hali halisi kabisa basi umeongezeka mara mbili zaidi ya ule unaotangazwa na Serikali, na hii Household Budget Survey hata Serikali inaitumia kwa hiyo, maana yake ni kwamba imeikubali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa mujibu wa Household Budget Survey masikini nchi hii wameongezeka kwa milioni 1.5 kutoka masikini milioni 11.4 mwaka 2001 hadi kufikia masikini milioni 12.9 mwaka 2007.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hata hapo unapozungumzia kiwango hicho cha kuongezeka ukitazama vigezo vyenyewe vilivyotumika ndiyo vinakuacha hoi, kwamba mtu ambaye anahesabiwa kuwa sio masikini nchini Tanzania ni yule ambaye akiwa Dar es Salaam ana uwezo wa kutumia shilingi 641/= au zaidi kwa siku, au akiwa ana uwezo wa kutumia shilingi 532/= au zaidi katika miji mingine na shilingi 469/= au zaidi katika vijiji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika sisi tuliomo humu ndani tujiulize, nani anaweza kuishi kwa shilingi 641/= Dar es Salaam kwa siku? Au Waheshimiwa Wabunge tupewe sisi shilingi 641/= tuambiwe tukaishi Dar es Salaam kwa siku tuone tunaweza kuishi katika hali gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa hakika ukitazama umasikini umeongezeka sana, na ukitumia kigezo cha Benki ya Dunia, ambapo mtu anahesabiwa kuwa ni masikini wa kutupwa iwapo anaishi chini ya dola moja kwa siku utagundua kwamba ukichanganya na hii Household Budget Survey basi asilimia 90 ya Watanzania ni masikini wa kutupwa na hao ni sawasawa na Watanzania milioni 36 kati ya Watanzania milioni 43 ambao tunao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii inasikitisha sana kwa sababu badala ya kuwasaidia wananchi hawa kunyanyuka sisi tunaendelea kuwakomoa kwa kodi kama zilivyoonekana hapa. Leo Serikali hii inatoa misamaha ya shilingi bilioni 752 ambazo wapinzani tumepiga kelele sana kwamba ipunguzwe angalau kwa 50% lakini mfanyakazi wa chini nafuu aliyopewa ni kuondolewa 1% katika kodi ya mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, yapo mengi sana ya kuthibitisha hoja kwamba katika miaka hii mitano (5) kwa hakika hali ya maisha ya Mtanzania imezidi kwenda chini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala jingine ambalo ningependa kulizungumzia hapa ni Ajira. Tunaambiwa kwamba, lengo la Ilani ya CCM lilikuwa ni kutoa ajira milioni moja katika kipindi cha miaka mitano hii. Tumewahi kupewa takwimu kwamba ajira hizo zimefikiwa na zimevuka kiwango, lakini kitu cha kufurahisha ukisoma Taarifa ya Hali ya Uchumi ambayo Waziri wa Fedha na Uchumi alitusomea hapa yeye mwenyewe anatuthibitishia katika ukurasa wa 6 kwamba, kwa mujibu wa utafiti wa ILFS kunakuwa na watu 760,000 wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka na katika hao ni 40,000 tu ndiyo wanaopata ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa takwimu hizi Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Uchumi anaziamini maana yake katika miaka mitano, 40,000 X 5 tumetengeneza ajira 200,000 na kwa hivyo, hizo ajira milioni 1 zilizoahidiwa hazipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na zaidi ukiangalia katika hotuba tulizoletewa katika sekta zote kama uvuvi, madini, miundombinu hali imeharibika kabisa. Leo katika miaka mitano (5) reli imekwama kufanya kazi. Nilikuwa nazungumza na Balozi mmoja wa nje hapa nchini siku moja akaniambia anashangaa reli hii ilikuwa inafanya kazi vizuri mwaka 1914, lakini leo mwaka 2010 Reli ya Kati haifanyi kazi, anashangaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini zaidi ATC ambayo haijawahi kufa tangu mwaka 1977 ilipoanzishwa kwa maana ya kuwa grounded, imekuwa grounded katika miaka mitano hii. Ukienda katika Bandari kila siku tunalalamikiwa kwamba hali imekuwa mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali hii tusidanganyane kuwa Serikali imetekeleza Ilani. Na kutokana na hali hiyo nasema siungi mkono hoja. Ahsante sana! (Makofi)

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: