ismailjussa

Katiba Mpya itakuja lini?

In Michango Bungeni on July 11, 2010 at 3:43 pm

 

MCHANGO WA MAANDISHI NILIOUTOA BUNGENI WAKATI WA MJADALA WA BAJETI YA OFISI YA WAZIRI MKUU – TAREHE 18 JUNI 2010

 

Mhe. Spika, wakati akijibu za wabunge waliochangia muswada wa Sheria ya kufanya marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi tarehe 12 Februari, mwaka huu, na akijibu mchango nilioutoa mimi siku ya kwanza nilioingia Bungeni, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Mhe. Philip Marmo, alikubaliana na hoja yangu kuwa muundo wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa unahitaji marekebisho kulingana na mahitaji ya mfumo wa demokrasia ya vyama vingi ambao sasa umetimiza miaka 18 hapa nchini tokea 1992 ulipoanzishwa.

Mhe. Spika, akilizungumzia suala hilo, alisema na naomba nimnukuu kutoka kwenye Hansard: “Muundo wa Tume; hili limeelezwa vizuri sana na Mheshimiwa Ismail Jussa Ladhu. Niseme tu kwamba, hoja hii imejitokeza mara nyingi; ni hoja nzito na siyo hoja ya kuipuuza hata kidogo. Isipokuwa hoja hii inagusa Katiba na sisi sote tunafahamu mchakato wa namna ya kubadilisha Katiba. Kwa hiyo, pendekezo na ombi langu kwa Wabunge wote na wadau wote ni kwamba, kwa vile muda uliobaki kati ya leo na Uchaguzi Mkuu siyo mrefu, ni muda mdogo sana uliobaki na haitawezekana mchakato huu kukamilika, basi jambo hili lishughulikiwe baada ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2010 kwa utaratibu wa kawaida wa mchakato wa kubadilisha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Mhe. Spika, namshukuru Mhe. Waziri kwa kukubaliana na hoja yangu wakati ule na pia nakubaliana naye kwamba muda uliobaki kati ya sasa na Uchaguzi Mkuu ni mdogo. Sasa basi naomba ahadi yake aliyoitoa kwa niaba ya Serikali ifanyiwe kazi ili mara baada ya Uchaguzi Mkuu, tuanze process hiyo. Isije ikawa tena tunasubiri hadi mwaka 2014 na 2015, hoja hii ije ijibiwe tena hivi hivi kwamba muda uliobaki ni mfupi.

Mhe. Spika, Watanzania kupitia taasisi mbali mbali zikiwemo vyama vya siasa, jumuiya na taasisi za kiraia, jumuiya na taasisi za kidini na jumuiya zisizo za kiserikali na mashirika ya kutetea demokrasia na haki za binadamu, wamekuwa wakitoa na kusisitiza madai na haja ya kuwa na Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakayokidhi matakwa ya demokrasia ya vyama vingi na pia inayokwenda na wakati na utashi na matarajio, yaani hopes and aspirations, ya Watanzania wa leo. Modernisation ni muhimu sana Mhe. Spika hasa ikizingatiwa kuwa Tanzania ni taifa la vijana. Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 70 ya Watanzania ni vijana wa umri wa miaka 30 na chini ya hapo. Hawa wanahitaji Katoba mpya inayokwenda sambamba na mahitaji yao ya leo na ya wakati unaokuja.

Mhe. Spika, nimuombe basi Mhe. Waziri Mkuu atakapokuja kufanya majumuisho ya mjadala hapa, atueleze ni vipi Serikali imejipanga baada ya uchaguzi kuhakikisha inakuja na mpango madhubuti utakaoanzisha mchakato wa kuandika Katiba mpya, kama ilivyoahidi kupitia kauli ya Waziri wa Nchi ya tarehe 12 Febnruari. Nasema hivi nikitambua kuwa Serikali ni endelevu, kwa hivyo wowote watakaokuwa madarakani watapaswa kutekeleza ahadi hii ya Serikali.

Mhe. Spika, nakushukuru sana.

 

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: